BIASHARA

NI MWENDO WA KUTIZAMA ANGANI, NDEGE MPYA AINA YA BOEING B737 – 9MAX KUTUA NCHINI

NI MWENDO WA KUTIZAMA ANGANI, NDEGE MPYA AINA YA BOEING B737 – 9MAX KUTUA NCHINI

Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Tanzania inatarajia kupokea ujio wa ndege mpya ya abiria aina ya Boeing B737-9MAX pamoja na uzinduzi wa ndege mbili za mafunzo aina ya Cessna 172S.


Waziri Profesa Mbarawa amesema Hafla ya mapokezi na uzinduzi wa ndege hizo itafanyika katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) tarehe 03 Oktoba,2023.


Amesema mwaka 2016, Serikali ilichukua hatua za kuifufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuanza kuinunulia ndege na kufanya mabadiliko ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi. Hadi Septemba, 2023 ATCL imeshapokea ndege 12 mpya ambazo zimenunuliwa na Serikali.


“Ndege hizi ni: ndege mbili kubwa aina ya B787-8 Dreamliner ambazo zinauwezo wa kubeba abiria 262 kila moja; ndege nne za masafa ya kati aina ya Airbus A220-300 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja; ndege tano za masafa mafupi aina ya D8 Q400 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na ndege kubwa ya mizigo aina ya B767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54.


Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt, Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuhahakikisha kuwa Kampuni ya Ndege Tanzania inatoa huduma zenye kuhimili ushindani kwa kuanzisha safari za moja kwa moja kwenda kwenye masoko ya kikanda na kimataifa. Mwezi Julai, 2021 Serikali iliingia mikataba na Kampuni ya Boeing ya Marekani ya ununuzi wa ndege nne mpya zenye teknolojia ya kisasa.


Ndege hizo ni ndege mbili za abiria za masafa ya kati aina ya B737-9MAX zenye uwezo wa kubeba abiria 181 kila moja, ndege moja ya abiria ya masafa marefu aina ya B787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na ndege moja kubwa ya mizigo aina ya Boeing B767- 300F yenye uwezo wa kubeba tani 54.

Ndege ya mizigo aina ya B767-300F tayari ilishawasili na inaendelea kutoa huduma zake na ndege moja ya masafa ya kati aina ya B737-9Max uundaji wake umekamilika na inatarajia kuwasili nchini tarehe 03 Oktoba, 2023. Ndege mbili zinaendelea kuundwa ambapo zinatarajia kuwasili nchini mwezi Disemba, 2023 na mwezi Machi, 2024.


Ndege ya abiria ya masafa ya kati aina ya B737-9MAX ambayo uundaji wake umekamilika inatarajia kuwasili nchini tarehe 03 Oktoba, 2023. Ndege hiyo inauwezo wa kubeba abiria 181 katika madaraja mawili ambapo daraja la kawaida “economy class” ni abiria 165 na daraja la biashara (business class) abiria 16, pia uwezo wa kubeba mzigo wa tani 6 na kuruka wastani wa saa 8 bila kutua.


Kuwasili kwa ndege hiyo kutaifanya ATCL kuwa na ndege 13 mpya zilizonunuliwa kutoka na utekelezaji wa mpango mkakati wa Serikali ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2016 na hivyo kuwa na ndege 14 zinazosimamiwa na ATCL katika uimarishaji wa wigo wa mtandao wa safari zake ndege kwa soko la ndani, kikanda na kimataifa.
Kwa sasa ATCL inahudumia vituo vya ndani vipatavyo 14 ambavyo ni Mwanza, Bukoba, Songea, Zanzibar, Katavi, Dar es Salaam, Iringa, Geita, Kigoma, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, na Tabora. Aidha, ATCL inahudumia vituo vya Kikanda na kimataifa ambavyo ni Entebbe- Uganda; Nairobi- Kenya; Bujumbura – Burundi; Hahaya-Comoro; LubumbashiDRC; Ndola, Lusaka – Zambia; Harare- Zimbabwe; Johannesburg – Afrika Kusini; Mumbai – India, na Guangzhoa – China na Dubai.
Ujio wa ndege hii ya kisasa ya masafa ya kati aina ya B737-9MAX kutaiwezesha ATCL kuongeza vituo vya Pemba, Tanga, Mafia, Nachingwea, na Musoma kwa mtandao wa safari za ndani.

Pia itaongeza miruko ya safari za usiku kwa viwanja vya ndege ambavyo vina taa pamoja na kuanzisha safari za usiku katika viwanja vya ndege vya Dodoma na Songea ambavyo miradi ya ufungaji wa taa za kuongozea taa imekamilika. Kwa upande wa mtandao wa safari nje ATCL itaendelea kuongeza miruko ya kwenda Mumbai, India na Guangzhou, China huku ikianzisha safari mpya za Kinshasa, Goma, Dubai, Muscat, na Lagos.
Sambamba na uimarishaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) tangu mwaka 2016 Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa ndege zinazonunuliwa zinakuwa na wataalamu wa ndani wa kuzihudumia ili kupunguza gharama za kutumia wataalam wa nje hususan Marubani na Wahandisi ndege.


Hatua hizo ni pamoja na kukijengea uwezo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kukijengea majengo, ununuzi wa mitambo na vifaa vya kufundishia, ununuzi wa ndege za mafunzo, na kuweka miundombinu wezeshi kwa ajili kutoa Kozi za muda mrefu za Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege (Degree and Diploma); Kozi za kutoa mafunzo ya Wahudumu wa Ndani ya Ndege (Cabin Crew) na Uendeshaji wa Safari za Ndege; Pamoja na Ndaki ya Chuo cha Urubani (Flight Crew).

About Author

Bongo News

1416 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *