KITAIFA

“KIPAUMBELE CHETU ARUSHA KIWE KAZI TU” – RC MAKONDA

“KIPAUMBELE CHETU ARUSHA KIWE KAZI TU” – RC MAKONDA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewataka watendaji na Viongozi wa ngazi zote za Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kufanya kazi kwa bidii katika kutimiza ahadi na maelekezo ya Chama na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Makonda ametoa kauli hiyo leo Mei 23,2024 ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara ya Kikazi Wilayani Longido, Ziara ambayo itafanyika kwa siku sita kwenye Wilaya zote za Mkoa wa Arusha.

Mara baada ya kupokelewa na watumishi wa Wilaya hiyo, Mhe. Makonda amesisitiza suala la Uwajibikaji na kusikiliza wananchi, akitaka kila mmoja kutambua majukumu yake na kuthamini kuaminika kwake na Serikali ya awamu ya sita, akihimiza pia ushirikiano kutoka kwa watumishi na watendaji mbalimbali ili kuleta matokeo ya haraka kwenye kuwatumikia wananchi wa Longido.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Longido Marko Henry Ng’umbi amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Bilioni 44 ndani ya miaka yake mitatu ya uongozi kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Longido.

Mhe. Ng’umbi amesema fedha hizo zimefanikisha kupeleka huduma ya nishati kwenye Vijiji vyote vya Longido pamoja na kusaidia miundombinu mbalimbali ya elimu, afya pamoja na barabara.

Akiwa Longido, Mhe. Mkuu wa Mkoa atakagua nyumba za watumishi wa afya Leremeta,atatembelea mradi wa Maji Sinya pamoja na kukagua shule ya Sayansi ya waaichana Longido kabla ya kufanya mkutano mkubwa wa hadhara kwenye uwanja wa shule ya Msingi Namanga.

Katika ziara yake Mhe. Paul Christian Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na maafisa wengine wa serikali na Chama Cha Mapinduzi wametumia magari maalumu yanayotumika kusafirisha watalii mkoani Arusha ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuutangaza utalii wa Arusha na kuendelea kuvutia zaidi watalii na wageni mbalimbali kuutembelea mkoa wa Arusha.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *