📌 Dkt. Biteko akutana na Balozi wa Japan nchini
📌 Tanzania na Japan kuendelea kuimarisha ushirikiano wake
📌 Dkt. Biteko aishukuru Japan kufadhili mradi wa umeme Singida
Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha, kuimarisha, kurahisisha na kuwezesha upatikanaji wa umeme na nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu ili kupunguza athari za kiafya, mabadiliko ya tabia nchi na kuboresha maisha ya wananchi.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Mei 9, 2025 ofisini kwake jijini Dar es salaam wakati alipotembelewa na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Youichi Mikami.
“ Serikali imedhamiria kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 21 hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2030 tumewashirikisha sekta binafsi ili kufikia azma hii,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Serikali imeandaa Mpango mahsusi wa Taifa wa Nishati kwa kipindi cha miaka mitano (National Energy Compact 2025 – 2030). Mpango ambao umeandaliwa kwa ushirikiano wa sekta binafsi na wameahidi kuchangia fedha mfano Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Dkt. Biteko amesema fedha hizo zitasaidia kufikia malengo ya Mpango huo wenye lengo la kuhakikisha watu milioni 300 waliopo kwenye Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara wanapata huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.
Katika mazungumzo yake na Balozi wa Japan, Mhe. Mikami Dkt. Biteko ameishukuru Serikali ya Japan kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa miradi ya umeme nchini.

“Tunawashukuru kwa ushirikiano wenu na kwa kufadhili mradi wa uunganishaji umeme kutoka Singida hadi nchini Kenya ambao tayari umekamilika. Tunapenda pia kushirikiana nanyi katika miradi ya gesi. Nchi zetu zimekuwa na ushirikiano mzuri na nia ya dhati ya kuhudumia wananchi wake” amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Youichi Mikami amesema kuwa nchi yake na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na kuwa Japan itaendelea kuimarisha uhusiano huo.

Pia, ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali (Mission 300) uliofanyika hivi karibuni ambao ulilenga kujadili kuhusu usambazaji wa nishati ya umeme barani Afrika.
1 Comment
I’ve been browsing online more than 2 hours today, yet
I never found any interesting article like yours. It is pretty worth enough for me.
In my opinion, if all webmasters and bloggers made good content as you did, the internet will be a lot more useful than ever before.