Mwanaharakati maarufu wa Kenya, Boniface Mwangi, ameachiwa huru na kurudishwa kwao baada ya kushikiliwa kwa siku kadhaa na vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania.

Mwangi alisindikizwa kutoka Tanzania hadi Ukunda nchini Kenya na kuachiwa akiwa salama salmini. Serikali ya Kenya na familia yake wamethibitisha kurejea kwake.
Mwanaharakati huyu mwenye historia ya kuhamasisha machafuko nchini Kenya aliingia nchini Tanzania mapema wiki hii kwa madai ya kuja kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, iliyosikilizwa Mei 19,2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, taarifa za kiintelijensia zinaonyesha lengo halisi la mwanaharakati huyo kuja nchini Tanzania lilikua kuchochea vurugu kwa mgongo wa kesi ya Lissu, kwa maslahi yake binafsi na ya wanaomtuma, kama ambavyo amekua akifanya nchini Kenya.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikemea vikali wanaharakati wanaoingia nchini kwa lengo la kuanzisha chokochoko, akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kulisimamia jambo hilo ili kudhibiti watu hao.