KITAIFA

RC MAKONDA AKERWA NA TABIA YA WATENDAJI KUTOTEMBELEA MIRADI YA MAENDELEO.

RC MAKONDA AKERWA NA TABIA YA WATENDAJI KUTOTEMBELEA MIRADI YA MAENDELEO.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameonya tabia ya baadhi ya watendaji wa serikali na taasisi zake kutotembelea miradi ya maendeleo suala ambalo limekuwa likisababisha wananchi kuteseka ma ukosefu wa huduma mbalimbali za kijamii licha ya serikali kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi hiyo.

Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda ametoa kauli hiyo mapema leo Mei 23, 2024 wakati alipotembelea Zahanati ya Kijiji cha Lemereta pembezoni mwa Mji wa Longido na kuelezwa kuhusu changamoto za ukosefu wa Umeme wa Uhakika na kutopatikana kwa maji kwenye zahanati hiyo iliyo muhimu kwa wakazi wa Kijiji cha Lemereta.

Bwana Supuk Melita Mwenyekiti wa kijiji cha Lemereta amemueleza Mhe. Mkuu wa Mkoa kwamba licha ya kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Maji vijijini na kwa Shirika la Umeme Tanesco Wilaya ya Longido, ni miezi mitatu sasa hawakuwahi kuona maafisa wa mamlaka hizo wakifika na kutatua changamoto walizowasilishiwa na wananchi.

Kufuatia hali hiyo, Mhe. Mkuu wa Mkoa amemtaka Bwana Ramadhan Musiba, Meneja wa Mamlaka ya Maji vijijini Wilaya ya Longido kumuandikia barua mteule wake (Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji) ili kueleza kuhusu udanganyifu alioutoa kwa Uongozi wa Mkoa pamoja na kushindwa kuwa mfuatiliaji mzuri wa miradi ya Maji inayotakiwa kusimamia na ofisi yake.

Katika Hatua nyingine Mhe. Makonda amemuagiza Bwana Lazaro Lenoi, Meneja wa Tanesco Wilaya ya Longido kuhakikisha kuwa ndani ya siku tatu Zahanati ya Lemereta inakuwa na Umeme wa kutosha ili kuondokana na changamoto ya Umeme kushindwa kuendesha vifaatiba na mashine nyingine zinazotumika kwenye Zahanati hiyo.

Mhe. Makonda amewataka watendaji kuwa na utamaduni wa kwenda kwa wananchi kila wakati na kutatua changamoto zao badala ya kukaa ofisini pekee na matokeo yake kusababisha ubadhirifu, uharibifu na kusuasua kwa miradi mingi ya maendeleo inayosimamiwa na serikali ya awamu ya sita.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *