Jumla ya wananchi 2,774,495 wakiwemo wanawake 1,390,535 na wanaume 1,381,960 wamepatiwa huduma za Msaada wa Kisheria tangu kuzinduliwa kwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa upande wa Tanzania Bara mwezi Machi 2023.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani Kusini Unguja uliofanyika katika viwanja vya Mtende-Azimio leo 10/05/2025 ambapo mgeni rasmi alikua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi.

Mhe. Sagini ameongeza kuwa migogoro 5,704 imetatutliwa kati ya migogoro 23,399 ya muda mrefu iliyoibuka huku migogoro 18,987 ikiwa katika hatua mbalimbali za utatuzi na utekelezaji wa kampeni tayari umefikia Mikoa 25, halmashauri 180 na vijiji/mitaa 8702 ya Tanzania bara huku mkoa uliosalia wa Dar es Salaam ukitarajiwa kukamilika mwezi Juni 2025.

Aidha Mhe.Sagini amesema kuwa wananchi waliofikiwa na kampeni hii wamepata huduma mbalimbali ikiwemo elimu ya haki na wajibu, umiliki na utatuzi wa migogoro ya Ardhi, utunzaji wa watoto, mirathi, ndoa na familia, utatuzi wa migogoro ya ajira na kazi, wosia pamoja na usajili wa matukio muhimu ya binadamu na haki za binadamu.

Ameongeza kuwa kutatuliwa kwa migogoro na elimu ya haki, uraia na Utawala Bora inayotolewa katika kampeni imesaidia kuleta Amani na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Aidha ameeleza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashirikiana na Ofisi ya Rais , Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora katika kuandaa taarifa kuhusu mikataba ya haki za binadamu za kikanda na kitaifa pamoja na kupitia mikataba na Sheria inayohusu ubadilishanaji wa wafungwa kati ya Tanzania na Nchi nyingine.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *