Uncategorized KITAIFA

CCM HAINA MASHAKA NA UTENDAJI KAZI WA WAZIRI MKUU-MAKONDA

CCM HAINA MASHAKA NA UTENDAJI KAZI WA WAZIRI MKUU-MAKONDA

Novemba 2, 2023

*Asema ni kiongozi mchapakazi na mtiifu, Chama kina matumaini makubwa.

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi Paul Makonda amesema CCM haina shaka na utendaji kazi wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwani ni kiongozi mchapakazi na mtiifu.

“…Katika utendaji wa kazi sisi upande wa Chama tuna matumaini makubwa na uwajibikaji na uaminifu wa Waziri wetu Mkuu Kassim Majaliwa, tumemuona katika maeneo mengi akisimamia shughuli mbalimbali za Serikali na nilipotoa agizo la Chama kwa Waziri Mkuu nilitaka agizo hilo lifike kwa mtu anayeweza kuleta matokeo chanya kwa Chama.”

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi amesema lengo la CCM chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Serikali inatimiza kile ambacho imepewa kukifanya kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi, hivyo wana matumaini makubwa na utendaji kazi wa Mheshimiwa Majaliwa.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Novemba 2, 2023) alipokwenda ofisini kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma. Amesema lengo la Chama ni kuhakikisha ndoto ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wote hususani wanyonge inafikiwa.

Amesema Waziri Mkuu ni mtendaji mtiifu, mwaminifu na kwamba maelezo yaliyotolewa kwake na CCM kuhusu kushughulikia migogoro ya ardhi tayari ameyapokea na ameanza kuyatekeleza. “Nina imani hata miezi sita tuliyompa inawezekana akatumia hata miezi mitatu tukapata ripoti.”

Kadhalika, Makonda amesema Chama kimemwagiza Waziri Mkuu kuwachukulia hatua wote ambao wataonekana kukwamisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Serikali. “Yeyote ambaye anabainika kufanya ubadhirifu wa mali za umma na Waziri Mkuu akabaini achukue hatua mara moja na Chama tumempa baraka zote.”

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema Serikali imepokea maelekezo ya Chama na kwamba itaendelea kuyafanyia kazi na kuhakikisha migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini inaendelea kushughulikiwa.

Akizungumzia kuhusu suala la udhibiti wa fedha za umma, Mheshimiwa Majaliwa amesema serikali itaendelea kulisimamia jukumu hilo ili fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zitumike ipasavyo na katika viwango vya ubora vinavyotarajiwa.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *