KITAIFA

100 KUTOKA JKCI WAPIGWA MSASA WA KUWAHUDUMIA WAGONJWA WA DHARURA NA MAHUTUTI

100 KUTOKA JKCI WAPIGWA MSASA WA KUWAHUDUMIA WAGONJWA WA DHARURA NA MAHUTUTI

Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kurugenzi ya Upasuaji wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Wataalamu wa magonjwa ya moyo 100 kutoka Kurugenzi ya Upasuaji ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamepatiwa mafunzo ya kuongeza ujuzi wa jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliipongeza Kurugenzi ya upasuaji kwa kuwa na wazo la kuikutanisha Kurugenzi nzima kupata mafunzo hayo kwani ni ya muhimu katika kuokoa maisha ya wagonjwa wengi wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Peter Kisenge akizungumza na watumishi wa Kurugenzi ya Upasuaji wanaoshiriki
mafunzo ya siku mbili ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wakati
akifungua mafunzo hayo leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

“Kumuhudumia mgonjwa aliye mahututi sio kazi ya mtu mmoja inahitaji timu ya wataalamu wa afya mbalimbali walio na mafunzo ya kiwango cha juu cha kuokoa maisha kama ambavyo Kurugenzi  yenu imekuwa ikifanya na kuongeza ujuzi mara kwa mara”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema ni muhimu kwa  mafunzo hayo ya siku mbili yakabadilishe  muenendo wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi na kupokea mawazo kwa kila mshiriki kwani huduma ya dharura inahitaji ushirikiano wa pamoja.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema hii ni mara ya pili kurugenzi hiyo kuandaa mafunzo hayo yanayohusisha mafunzo kwa vitendo ili kila mtaalamu wa afya aweze kuona kwa uhalisia vifaa vinavyotumika na kufanya mazoezi kwa vitendo.

Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Angela Muhozya akitoa neno na shukrani wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku
mbili ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanayotolewa kwa
wafanyakazi wa Kurugenzi hiyo leo jijini Dar es Salaam.

“Wakati wa upasuaji mgonjwa anaweza akabadilika na kuhitaji matibabu ya dharura hivyo kama wahusika wakuu wa huduma za upasuaji lazima kila mfanyakazi ajue ni kitu gani kinatakiwa kufanyika ili kuokoa maisha ya mgonjwa”, alisema Dkt. Angela.

Dkt. Angela alisema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kusaidia wataalamu wa Kurugenzi ya Upasuaji kuwa katika viwango vya kimataifa vya kutoa huduma inayoendana  na maendeleo ya sayansi na teknolojia yaliyopo.

Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau akichangia mada wakati wa mafunzo ya siku
mbili ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanayofanyika katika
Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

“Mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi ni ya muhimu kwetu sisi kwasababu tunaamini kama wataalam wa afya tunatakiwa tuweze kuwa na utayari wa kuwahudumia wagonjwa wakati wowote”, alisema Dkt. Angela.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na msimamizi wa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) Lucia Kabeya akieleza jinsi wanavyowahudumia wagonjwa wanaolazwa katika wodi hiyo wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Washiriki wa mafunzo hayo ni wataalamu kutoka Hospitali ya  JKCI Dar Group, madaktari wa upasuaji, wataalam wa kuendesha mashine mbadala wakati wa upasuaji, wauguzi wanaofanya kazi katika chumba cha upasuaji na chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) na wauguzi wanaojifunza kuwahudumia wagonjwa wa dharura.

About Author

Bongo News

19 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *