KITAIFA

CHONGOLO: HATUTARUDI NYUMA, NI MBELE KWA MBELE

CHONGOLO: HATUTARUDI NYUMA, NI MBELE KWA MBELE

Kufuatia maneno yanayoendelea kuhusiana na uwekezaji wa uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam imeelezwa kuwa maoni ya wananchi yatakusanywa, yale yatakayoonekana yana tija yataingizwa kwenye mjadala wa mkataba ukaoingiwa kwenye uendeshaji huo wa bandari, lakini suala la Serikali kurudi nyuma ni mwiko, bali mambo yatakuwa ni mbele kwa mbele.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Komredi Daniel Chongolo alipokuwa anahutubia kwenye mkutano wa hadhara Wilayani Korogwe, Mkoani Tanga leo Julai 19, 2023 kuhusiana na sakata la bandari na mambo mengine ya maendeleo ambapo amesema kuwa lazima wananchi wasikilizwe huku Serikali ikitafuta tija na matokeo mapana kwa nchi na sivinginevyo.

 “Rais Samia alikuta ujenzi wa daraja la Busisi uko chini ya asilimia 30, sasa hivi umefika mbali kwasababu ni miradi ameikuta ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi, lazima kazi iendelee na kuendelea kwake ni kuitekeleza,  hawa wanaotugombanisha mbona hawasemi kule tuache, mbona hawasemi kule tunapeleka pesa nyingi haina tija, hawasemi maneno mengine, wameshikilia hili moja tu,” amesema Chongolo.

Aliendelea kuwa, “Kwasababu wanajua tukifanikisha hili tija yake itatupeleka mbele kwa spidi na wao watakosa mahali pa kunyooshea kidole ili waweze kuaminika na wananchi wakati wa uchaguzi ujao, hiyo ni akili ya Abunuazi. Ndugu zangu mtu anayekupenda anakushauri mambo ya msingi, lakini ukiona anakuja adui yako na kukushauri jambo, lazima uchukue kwa sura mbili, nenda kajiridhishe kwa kufanya utafiti wa kina kwasababu mara nyingi adui hawi na nia njema, waswahili walituasa ukiona adui yako anakupigia makofi wakati unafanya jambo, lishikilie vizuri, liangalie vema lazima litakuwa na changamoto mahali”.

Chongolo aliendelea kusema kuwa “Adui hawawezi kukupigia makofi na kukushangilia wakati unafanya jambo kama halina madhara, kwasababau ni adui muda wote anakutakia mabaya, akikushangilia maana yake ameshaona kuna kichaka unaenda kuzama, kuna shimo linakupeleka kuzama. Lakini ukiona adui yako anapiga kelele, analalamika, anatapatapa anatunga uongo, hapati usingizi, anatumia lugha mbalimbali zikiwemo za matusi  kuhangaika na hilo jambo, lishike linatija”.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *