KITAIFA

DED HAI AELEKEZWA KUMLIPA FUNDI ANAYEJENGA MIUNDOMBINU YA SHULE YA MSINGI MLIMA SHABAHA “B”

DED HAI AELEKEZWA KUMLIPA FUNDI ANAYEJENGA MIUNDOMBINU YA SHULE YA MSINGI MLIMA SHABAHA “B”

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasili kukagua miundombinu ya elimu katika Shule ya Msingi Kyuu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.
Deogratius Ndejembi amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Hai Bw. Dionis Myinga kumlipa fundi aliyepewa kandarasi ya
kujenga miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa na jengo la utawala
katika Shule ya Msingi Mlima Shabaha “B” kupitia mradi wa BOOST ili
akamilishe ujenzi kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mroma mara baada ya kukagua miundombinu ya elimu katika shule hiyo kongwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Hai.


Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo, akiwa Wilayani Hai wakati
akikagua ujenzi wa miundombinu ya elimu katika Shule ya Msingi Mlima
Shabaha “B” mara baada ya kubaini kasi ndogo ya ujenzi iliyosababishwa
na Halmashauri kutomlipa fundi madai ya fedha zake.
Mhe. Ndejembi ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kulipa
uzito suala la usimamizi na ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya
elimu, kwani Serikali imepeleka fedha nyingi ili ikamilike kwa wakati na
hatimaye wanafunzi wanufaike kwa kupata elimu bora.
“Fedha hizi zimeletwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuwawezesha mafundi kukamilisha
jukumu la ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa manufaa ya taifa,” Mhe.
Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi amewata watendaji Serikalini kusimamia kikamilifu
utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa uzalendo
kama ambavyo Mheshimiwa Rais anavyopambana kutafuta fedha ya ujenzi
wa miundombinu hiyo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akielekea kukagua miundombinu ya elimu katika mojawapo ya Shule kongwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Hai.


Kwa upande wake, Mbunge wa Hai Mhe. Saasisha Mafuwe amesema
kumekuwa na changamoto ya mafundi kutolipwa kwa wakati licha ya
Serikali kuwasilisha fedha katika Halmashuri ya Hai hivyo ameutaka
uongozi wa Halmashauri hiyo kutekeleza maelekezo ya Mhe. Ndejembi ili
wananchi wanufaike na miundombinu ya elimu inayojengwa.
Sanjari na hilo, Mhe. Mafuwe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipatia

Halmashauri ya Wilaya ya Hai ili kujenga miundombinu ya elimu na
barabara.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mhe. Amiri Mkalipa amesema kuwa
amepokea maelekezo ya Mhe. Ndejembi na kuongeza kuwa yeye pamoja
na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama watahakikisha ujenzi wa
miundombinu ya elimu unatekelezwa usiku na mchana ili Halmashauri ya
Hai isiwe ni kikwazo cha jitihada za Serikali kuboresha elimu nchini.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *