KITAIFA

DKT. MPANGO AFUNGUA BARABARA YA LOLIONDO-MTO WA MBU

DKT. MPANGO AFUNGUA BARABARA YA LOLIONDO-MTO WA MBU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria uzinduzi wa barabara ya Wasso – Sale yenye kilometa 49 wakati akiwa ziarani katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha Mei 17, 2023.

Makamu wa Rais Dkt. Phillip Isdor Mpango amefungua Barabara ya Loliondo–Mto Wa Mbu (km 217) Sehemu ya Wasso-Sale (km 49) ambayo imekamilishwa na Serikali kupitia TANROADS kwa kiwango cha lami wilayani Loliondo mkoani Arusha.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kushuhudia barabara hiyo ikifunguliwa, Makamu wa Rais Dkt Mpango amesema pamoja na kwamba gharama za ujenzi wa barabara ni kubwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itahakikisha inajenga kipande kilichobaki kwenda Mto wa Mbu.

Kwa kuanzia Makamu wa Rais Dkt Mpango ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha kuwa inaweka kwenye Bajeti ya wizara hiyo itakayosomwa Jumatatu Mei, 22-2023 na kuomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa kipande kingine korofi cha barabara km 24 kutoka Ngaresero kwenda Engaruka wakati Serikali kupitia TANROADS ikiendelea na mchakato wa Ujenzi wa sehemu nyingine ya barabara hiyo.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Geoffrey M Kasekenya amesema barabara hiyo ni muhimu kwa wananchi wa mkoa wa Arusha, wilaya ya Ngorongoro, Loliondo na vijiji vyote ambavyo barabara hiyo inapita na kwamba inahitajika sana na watalii wanaokwenda Mbuga ya Serengeti, lengo likiwa ni hadi kufikia mwaka 2025 mikoa yote iwe imeunganishwa na barabara nzuri kwa kiwango cha lami.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiweka jiwe la msingi uzinduzi wa barabara ya Wasso – Sale yenye kilometa 49 wakati akiwa ziarani katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha Mei 17, 2023.

“Naomba niwape Wananchi hawa Taarifa, Rais ametoa maelekezo, kipande cha km 10 kutoka Wasso kwenda Makao makuu Loliondo nacho kipo kwenye hatua ya manunuzi ili kijengwe kwa kiwango cha lami, Mtu akitoka makao makuu ya wilaya anakuja Wasso anaendelea na lami” ameongeza Naibu Waziri Kasekenya

Akitoa taarifa fupi ya Mradi huo Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng: Rogatus Mativila amesema Ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha mtandao wa barabara nchini kwa kujenga Barabara Kuu na za Mikoa kwa kiwango cha lami.

Amesema kusudio la kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ni kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji, kupunguza muda wa usafiri na usafirishaji wa mazao na mifugo kutoka ukanda huo hasa wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro katika mji wa Loliondo na vitongoji vyake ili kuongeza thamani ya mazao na mifugo na kukuza kipato kwa Wananchi waishio maeneo hayo, hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii katika nchi hasa katika Hifadhi za Taifa za Serengeti na Ngorongoro.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa mavazi ya kiongozi wa kabila la wasonjo wakati wa uzinduzi wa barabara ya Wasso – Sale yenye kilometa 49 wakati akiwa katika ziarani hiyo Mei 17, 2023.

Eng: Mativila ameeleza kuwa Mkandarasi aliyejenga sehemu ya kwanza ya Wasso – Sale ni Kampuni ya China Wu Yi Co. Ltd ya China kwa gharama ya Shilingi Bilioni 87.126, na kwamba mradi huo ulisimamiwa na TANROADS kupitia kitengo chake cha Uhandisi kiitwacho TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU).

Aidha utekelezaji wa Mkataba wa kipande hicho cha barabara umegharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100, na mradi ulitoa jumla ya ajira 426 kwa wazawa na 21 wafanyakazi wa kigeni.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *