Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda ametangaza kiama kwa Watu wanaokwepa Kodi na kutangaza Donge nono kwa watu watakaowafichua wakwepakodi na kukomboa Kodi.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Tuzo ya Mtoa Taarifa uliofanywa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji jana tarehe 08.05.2025 Jijini Dar es Salaam.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema kupitia Tuzo hiyo wananchi wanaombwa kutoa taarifa za watu wanaokwepa Kodi na kiasi kitakachokombolewa, mtoa taarifa atapatiwa asilimia tano, pia mtoa taarifa anaweza kupatiwa cheti cha Shukrani au kiasi cha fedha kwa taarifa ambazo zinahusisha masuala ya kinidhamu.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema wanafahamu wapo wenye Viwanda wanaowauzia Wafanyabiashara bidhaa bila kuwapatia risiti hali inayosababisha Wafanyabiashara hao washindwe kutoa risiti wanapouza bidhaa zao na kuwataka wajisalimishe kabla hawajafikiwa.

Aidha amewataka Wafanyabiashara wenye kipato cha Sh. Milioni 4 kwa mwaka kujisajili kwaajili ya kuanza kulipa Kodi wakiwemo wanaofanya biashara mtandao na kuwa TRA haitawafumbia macho watakaobainika kukwepa Kodi kwa kuwatoza Riba na adhabu tangu walipoanza kufanya biashara zao.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema watu wanaokwepa Kodi wanawanyonya wenzao wanaolipa Kodi kikamilifu maana wanaondoa usawa katika ulipaji wa Kodi na kuharibu ushindani wa biashara jambo ambalo siyo la kuvumiliwa.

Wakati wa uzinduzi wa Tuzo hiyo ya Mtoa Taarifa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Stanislaus Nyongo amesema Tuzo hiyo itawaibua wakwepakodi na kuleta Tija kwa Taifa.

Ametoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa za wakwepakodi.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *