KITAIFA

PROFESA MKENDA AFUNGUKA” TAIFA LINAHITAJI WALIMU BORA NA MAHIRI

PROFESA MKENDA AFUNGUKA” TAIFA LINAHITAJI WALIMU BORA NA MAHIRI

Raisa Said,Korogwe

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema Taifa linahitaji Walimu bora na mahiri katika kufundisha pamoja na uwezo wa kukaa na kuwalea vizuri watoto wa Kitanzania ili wafikie malengo yao na kusaidia nchi katika nyanja mbalimbali.

Profesa Mkenda  aliyasema  hayo Jana wilayani Korogwe   Mkoani  Tanga wakati akifungua Mafunzo ya Kitaifa kuhusu Uongozi, Usimamizi wa Shule na Utawala bora pamoja na kuwajengea uwezo Walimu Wakuu wa Shule za Msingi 347, kutoka Wilaya ya Korogwe Mji, Korogwe Vijijini na Lushoto ambapo alieleza kuwa Ualimu ni moja ya taaluma muhimu  na msingi mama kwa Maendeleo ya Taifa. 

“Tunahitaji  kuwasaidia Walimu kujiendeleza Kitaaluma, Hivyo kwenye Sera sasa hivi itakuwa ni lazima anayemaliza chuo cha Ualimu aende akafanye mazoezi ya kazi kwa mwaka mmoja apimwe ili aweze kuhitimu kama kada nyingine zinavyofanya” alisema Waziri Mkenda nakuongeza kuwa hawataki ualimu uvamiwe.

Prof. Mkenda ameeleza kuwa mageuzi ya Elimu ndio agenda kubwa Duniani, na kwamba tayari Serikali ilishaanza kufanyia kazi mageuzi hayo ili kuendana na wakati pamoja na kukidhi mahitaji ya sasa  na baadae ya Taifa na kitaifa.

Aidha amesisitiza kuwa azma ya Serikali ni kurudisha heshima ya Ualimu na kuhakikisha  wanapata walimu wenye sifa stahiki, bora, wenye uwezo na umahiri wa kufundisha na kulea watoto kwa kuzingatia maadili ya Kitanzania.

Hata hivyo ameongeza kuwa Serikali itaendelea kufanya juhudi kuhakikisha Walimu wanathaminiwa katika kutenda kazi ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu mbalimbali, kununua vifaa  ikiwemo  vishkwambi na kuweka mazingira rafiki katika utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema mpaka sasa Walimu wamefanya kazi kubwa, na kwamba bado kuna kazi kubwa zaidi inawahitaji kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023.

” Ni ukweli usiopingika Walimu ndio tegemeo letu kubwa sana hapa Nchini, mmechangia kwa kiasi kikubwa mageuzi makubwa yanayofanyika katika Elimu yetu, bila nyie hatuna elimu” Alieleza Mkenda.

Kwaupande wake  mtendaji mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Dkt. Siston Masanja alieleza kuwa  mafunzo hayo yanatekelezwa kwa awamu ya pili, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Shule za Awali na Msingi (BOOST) kupitia afua namba 8 ambayo ADEM ilipewa jukumu na Wizara ya Elimu,  kuendesha mafunzo kwa Walimu Wakuu 17,000 Nchini hasa kwa Tanzania Bara.

Ameeleza kuwa awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ilitekelezwa kati ya mwezi Septemba na Oktoba 2023 ambayo ilihusisha kati ya Walimu Wakuu 4,522 kutoka Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Njombe, Songwe, Morogoro, Dodoma na mkoa wa Mara.

“Awamu hii jumla ya Walimu Wakuu 4,620 kutoka Mikoa 6 ya Tanzania Bara watapatiwa mafunzo ikiwemo kutoka Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Kigoma, Mtwara, Simiyu na Mbeya. Zoezi hili litaendelea kwa Mikoa iliyobaki” alisema Dkt. Masanja.

Mkuu wa wilaya ya Korogwe William  Mwakilema  ameishukuru Serikali kuendelea kuimarisha miundombinu ya Elimu kuanzia Elimu ya Awali mpaka Vyuo, na kwamba imeendelea kuchagiza maendeleo katika wilaya hiyo na mkoa wa Tanga kwa ujumla.

Hata hivyo Walimu wanaopatiwa mafunzo hayo Kwa upande wao  Mwenyekiti wa mafunzo hayo wameahidi watatumia vema ujuzi na maarifa watakayoyapa katika kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya Wanafunzi na jamii kwa ujumla.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *