KITAIFA

JKT,  WIZARA YA KILIMO WASAINI MKATABA WA MASHIRIKIANO KUINUA SEKTA YA KILIMO

JKT,  WIZARA YA KILIMO WASAINI MKATABA WA MASHIRIKIANO KUINUA SEKTA YA KILIMO

Jeshi la kujenga Taifa (JKT) na Wizara ya Kilimo wametiliana saini mkataba wa mashirikiano katika kutekeleza mradi wa mashamba makubwa ya kuwawezesha vijana kufanya kilimo biashara ‘Building a Better Tomorrow’ (BBT) mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajab Mabele alisema jeshi hilo limeanza kutekeleza agizo la Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha vijana wanaotoka makambini wanajengewa Uzalendo wa Kitaifa na kunufaika na fursa zilizopo katika sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kupitia mradi huo wa BBT unaosimamiwa na Wizara ya Kilimo.

Mabele aliyasema hayo kwenye kilele cha maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane 2023 jijini Mbeya baada ya hotuba ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo alisema kuwa lengo ni kuhakikisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaungana na Wizara ya Kilimo ili vijana wa kitanzania wanaoandaliwa katika utaratibu wa BBT wawe katika wizara hizo mbili.

”Tutahakikisha kwanza wanapata Uzalendo katika Jeshi la Kujenga Taifa na ukakamavu ili wanapokwenda katika kazi zile ambazo zitakuwa za shamba waweze kuwa na uvumilivu,” alisema Meja Jenerali Rajab Mabele.

Kwa upande wake mkuu wa huduma za sheria kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Projest Rutaihwa alisema kuwa kupitia maonesho hayo wameweza kusaini makubaliano na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kwamba mashirikiano hayo ni katika taratibu za BBT ambazo zimezinduliwa hivi karibuni na Serikali huku wao Jeshi la Kujenga Taifa katika makubaliano hayo na wizara hizo watakuwa wanachukua vijana wanawafundisha Uzalendo, Ukakamavu na Stadi za Kazi.

Aidha Rutaihwa alisema kuwa kwa pamoja watakauwa wanaratibu uendeshaji wa mafunzo hayo na wanategemea mashirikianao hayo yatafikia pazuri. Vilevile Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Sarah Mwaipopo alisema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika utatuzi wa migogoro ikiwemo ya ardhi.

”Sisi tupo hapa kwasababu tunasimamia masuala ya utatuzi wa migogoro ikiwemo ya ardhi ambayo huwa inajitokeza mara kwa mara, hivyo ofisi yetu inahakikisha kwamba changamoto hizo zinaondolewa,” alisema Sarah. ­­

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *