KITAIFA

PSSSF: WAKULIMA NA WAFUGAJI NI WADAU WAKUBWA WA MFUKO KWENYE UWEKEZAJI WETU KATIKA VIWANDA

PSSSF: WAKULIMA NA WAFUGAJI NI WADAU WAKUBWA WA MFUKO KWENYE UWEKEZAJI WETU KATIKA VIWANDA

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesema Maonesho ya mwaka huu ya Nanenane yana maslahi mapana kwa Mfuko huo kutokana na uwekezaji ambao umefanya kwenye maeneo ya kilimo na mifugo, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. James Mlowe amesema.

Bwana Mlowe amebainisha hayo leo Agosti 3, 2023 kwenye Banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane 2023 yanayofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Alisema Mfuko unayo majukumu manne ambayo ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kisha kulipa mafao.

“Katika eneo hili la Uwekezaji, Mfuko umewekeza kwenye maeneo mbalimbali mojawapo ni eneo la viwanda, eneo hili tumewekeza kwenye kiwanda cha Kuchakata Tangawizi, Mamba Miamba kilichoko Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro na Kiwanda cha Chai Mponde, kilichoko Wilayani Lushoto Mkoani Tanga.”Alisema na kuongeza  kuwa PSSSF imewekeza kwenye Machinjio ya Kisasa Nguru Wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro, kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro (KLIC), na hii ni fursa kwa wafugaji.” Alifafanua Bw. Mlowe.

Alisema kwa sababu hiyo Wakulima na Wafugaji ni wadau muhimu wa Mfuko na kuwataka watembelee kwenye banda la PSSSF ili kujua fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye Mfuko katika maeneo hayo ya uwekezaji kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo.

Akizungumzia kuhusu majukumu mengine ya msingi ya Mfuko, Bw. Mlowe alisema PSSSF inatoa huduma kwa Watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ambayo Serikali inamiliki hisa zaidi ya asilimia 30%

“Hata kaulimbiu ya mwaka huu ya ‘Vijana na Wanawake ni Msingi imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula’ inatuunganisha,  tunapokuwa na chakula cha kutosha tunajenga nguvu kazi imara ambayo ni vijana na hawa wanapoajiriwa Serikalini wanakuja kuwa wanachama wetu.” Alifafanua Bw. Mlowe.

Akieleza zaidi ushiriki wa Mfuko katika Maonesho hayo alisema “Hapa bandani ni ofisi kamili, tunawahudumia wanachama wetu kama ambavyo wanavyohudumiwa kwenye ofisi zetu zilizoeneo nchi nzima Tanzania Bara na Zanzibar.” Alifafanua.

Alisema wanachama wakiwemo wastaafu wakitembelea kwenye banda hilo watakutana na watumishi wanaojali mteja, waaminifu na wenye weledi na utayari wa kuwahudumia na wataweza kupata Taarifa kuhusu Michango, Taarifa za Mafao yatolewayo na Mfuko, Taarifa za Uwekezaji lakini pia wastaafu wataweza kujihakiki kwa njia ya alama za vidole (Biometric).

Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa PSSSF, Bi. Grace Kabyemela, amewahakikishia Wanachama wakiwemo Wastaafu kuwa Mfuko uko katika hali nzuri ya kuhakikisha wanapata mafao yao kwa wakati kwa mujibu wa Sheria.

“Sheria inatutaka kuwa mwanachama anayestaafu anapowasilisha nyaraka zilizokamilika anapaswa awe amelipwa mafao yake ya mkupuo ndani ya siku 60, lakini sisi PSSSF tumejiwekea malengo ndani ya siku 30 tunafanya malipo.” Alidokeza Bi.Kabyemela.

Aidha kuhusu malipo ya pensheni ya kila mwezi, Bi. Kabyemela alisema Mfuko unahakikisha ikifika tarehe 25 ya kila mwezi wastaafu wanakuwa wamelipwa pensheni zao mwezi.

Habiba Khalid Mhina yeye ni Mwanachama wa PSSSF ambaye alitembelea banda la PSSSF ili kupata taarifa za michango yake na baada ya kuhudumiwa aliipongeza PSSSF kwa kumpatia taarifa zake kwa haraka

“Mimi ni Mfanyakazi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dodoma, nimefika banda la PSSSF kupata taarifa za michango na kwakweli chini ya dakika 5 nimepata huduma na kukabidhiwa taarifa ya michango yangu.” Alisema.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *