KITAIFA

RAIS SAMIA: AFRIKA SIO SALAMA KWA WALA RUSHWA

RAIS SAMIA: AFRIKA SIO SALAMA KWA WALA RUSHWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi wa Taasisi mbalimbali, Wanafunzi pamoja na Wananchi wakati wa Kilele cha
Maadhimisho ya Siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika yaliyofanyika katika ukumbi wa Nyasa uliopo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC Jijini Arusha tarehe 11 Julai, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa ni mfumo wa kisheria unaoziwezesha nchi kushirikiana katika kuzuia vitendo vya rushwa, katika kuwachunguza watuhumiwa wa makosa ya rushwa pamoja na urejeshwaji wa mali zilizotokana na vitendo vya rushwa katika nchi husika, kubadilishana watuhumiwa wa makosa ya rushwa waliotoroka nchi zao na kubadilishana taarifa na ushahidi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC Jijini Arusha kwa ajili ya Kilele cha Maadhimisho ya
Siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika tarehe 11 Julai, 2023.

Aidha, Mkataba huo umeweka misingi ya kisheria ya nchi za Afrika  kushirikiana katika mafunzo ya kiweledi yanayohusu namna ya kuzuia na kupambana na rushwa na kupeana misaada ya kisheria pamoja na ushirikiano wa kiufundi katika kushughulikia kwa haraka maombi ya vyombo vyetu tulivyovipa jukumu la lazima la kuzuia, kutambua, kuchunguza na kuadhibu washtakiwa wa makosa ya rushwa.

Hayo yamelezwa leo Julai 11, 2023 jijini Arusha na Mhe. Rais Samia wakati akihutubia katika Kilele cha Maadhimisho ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya maua kutoka kwa Kiongozi wa Girl Guide wa Arusha Annasia Vincent Cosmas mara baada ya kuwasili kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC Jijini Arusha kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika tarehe 11 Julai, 2023.

“Natoa rai kwa wadau wote wa mapambano dhidi ya rushwa kutafakari na kuchambua kwa dhati masuala haya ili kubainisha changamoto au vikwazo vya mapambano haya na kuchukua hatua muafaka, wala rushwa wanapaswa kufahamu kwamba nchi zetu si vichaka vya kuficha fedha zilizotokana na rushwa au kufuga wala rushwa. Tunataka dunia nzima ifahamu kuwa, Afrika sio salama kwa wala rushwa, na hilo lionekane kwa vitendo kupitia hatua tunazozichukua dhidi ya wala rushwa na sio mikutano, makongamano na maneno peke yake”, alisema Rais Samia.

Alifafanua hatua iliyopigwa na Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kusema kuwa, Tanzania imewekeza zaidi katika matumizi ya mifumo ya teknolojia ya habari kwa huduma ambazo si lazima yawepo mawasiliano ya mtu na mtu ili kupunguza tatizo la kuzungumza na kupatana, na kuwa tayari Tanzania inatumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika michakato mbalimbali ikiwemo ya zabuni, usajili wa biashara, namba ya mlipa kodi na maombi ya kuunganishiwa umeme.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna wa Polisi (CP) Salum Hamduni kuhusiana
na kazi mbalimbali ambazo Taasisi hiyo inafanya kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika yaliyofanyika katika ukumbi wa Nyasa uliopo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC Jijini Arusha tarehe 11 Julai, 2023.

“Pamoja na juhudi hizi, bado jitihada zinahitajika kukabiliana na janga la rushwa kwa njia za kiuadilifu na ufanisi zaidi, hivyo imeanzishwa divisheni ya Mahakama Kuu inayosikiliza kesi zinazowahusu washtakiwa wa makosa ya rushwa kubwa. Kwa kuanzia mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2021/22, tulifanikiwa kuokoa na kudhibiti matumizi ya fedha yasiyostahili ya zaidi ya shilingi bilioni 139, hiki ni kiasi kikubwa kwa fedha za umma”, alibainisha Rais Samia.

Viongozi wa Dini, Maafisa kutoka Taasisi mbalimbali, Wanafunzi pamoja na Wananchi wakiwa kwenye ukumbi wa Nyasa uliopo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
AICC Jijini Arusha kwa ajili ya Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika tarehe 11 Julai, 2023.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika, Paschal Antonio Joachim alisema kuwa miaka 20 iliyopita, Umoja wa Afrika ulifanya maamuzi muhimu kwa kuidhinisha makubaliano  ya kuwa na chombo cha pamoja  ambacho kimewekwa kama mfumo wa nchi za Afrika ili kuweza kudhibiti na kupambana na rushwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akinyanyua juu Tuzo kutoka Bodi ya Ushauri ya Kupambana na Rushwa Afrika mara baada ya kukabidhiwa
wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika yaliyofanyika katika ukumbi wa Nyasa uliopo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC Jijini Arusha tarehe 11 Julai, 2023.

“Tunaendelea kufanya shughuli zetu ili tuweze kuwa na Afrika tunayoitaka sisi, ambayo ina Demokrasia, Utawala Bora, inaheshimu Haki za Binadamu na Utawala wa Sheria. Aidha, ninampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuchukua muda wake na kushiriki katika Maadhimisho haya ya Kupambana na Rushwa Afrika”, alimaliza Joachim.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *