BURUDANI

SANAA ITUMIKE KUWAUNGANISHA WATANZANIA BILA KUJALI TOFAUTI ZAO

SANAA ITUMIKE KUWAUNGANISHA WATANZANIA BILA KUJALI TOFAUTI ZAO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amefunga Tamasha la 42 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo akisisitiza kuwa Sanaa ina uwezo mkubwa wa kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti za kabila, dini na maeneo wanayotoka.

Akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kufunga tamasha hilo Oktoba 28, 2023 mjini Bagamoyo, Dkt. Biteko amewasihi wasanii wote nchini watengeneze kazi za Sanaa zinazohimiza watu kupenda utu na kufanya kazi ili kuendeleza kujenga taifa lenye taswira njema linalotambuliwa kwa utamaduni wake.

“Ninyi Wasanii wa Tanzania, kwa kushirikiana na taasisi yetu hiii ya Sanaa Bagamoyo endeleeni kutengeneza kazi za Sanaa zinazojenga umoja na uzalendo, kuhimiza Watanzania kupenda kazi ambayo ni kipimo cha Utu” amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye ambaye alimwakilisha Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amesema Tamasha hilo limekuwa kwa matokeo mzuri na wananchi wanajitokeza kwa wingi kwa kuzingatia linasimamiwa na Wizara ya furaha na wananchi wataendelea kupata burudani kupitia kazi za Sanaa na michezo.

Naye Mkuu wa mkoa wa Pwani Bw. Abubakari Kunenge amesema mkoa huo umejipanga vizuri na mazingira ya mkoa huo ni usalama, yapo vizuri na amewahakikishia washiriki usalama wao wakati wote wa tamasha hilo akiwakaribisha watembelee maeneo yote ya mji ya kihistoria ya Bagamoyo ambayo yamesheheni historia na vivutio lukuki vya utalii.

Tamasha hilo limehusisha maonesho ya sanaa za jukwaani ikiwemo ngoma za asili na za kisasa, muziki wa asili na wa kisasa, maigizo, sarakasi, ushairi, vichekesho na mazingaombwe kutoka Tanzania na vikundi vya Kimataifa kutoka nchi za Canada, Botswana, Afrika Kusini, Uganda, Zambia, Burundi, na Kenya.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *