KITAIFA

TANZANIA NA ALGERIA KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI

TANZANIA NA ALGERIA KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Watu wa Algeria zimesisitiza umuhimu wa kukuza
diplomasia ya uchumi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa
Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya
Nchi hizo mbili ngazi ya Maafisa Waandamizi unaoendelea jijini
Algiers, Algeria.
Mkutano huo utafuatiwa na Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu
utakaofanyika tarehe 31 Agosti 2023 ambapo kwa pamoja mikutano
hiyo inafanya maandalizi ya Mkutano Ngazi ya Mawaziri utakaofanyika
tarehe 1 Agosti 2023.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano ngazi Wataalam umeongozwa na
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na kwa upande wa Algeria
umeongozwa na Mkurugenzi Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje
ya Algeria, Balozi Selma Haddadi Malika.
Akifungua mkutano huo Balozi Shelukindo ameeleza kuwa ushirikiano
uliopo kati ya Tanzania na Algeria ni wa kihistoria na uliojengwa katika
misingi imara na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwl. Julius
Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Ahmed Ben Bella.
Pia amesema Tanzania imejikita katika mageuzi ya kisekta hususan
katika sekta za kilimo, utalii na taasisi za fedha ili kuiwezesha sekta
binafsi kukuza uchumi wa Taifa. Pia inaendelea na ujenzi wa
miundombinu ili kurahisisha mawasiliano kupitia usafiri wa barabara,
reli, maji na anga.
‘’Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo wa kuimarisha sekta za

uzalishaji na kuweka mpango wa usimamizi katika masuala ya biashara,
uwekezaji na uchumi wa viwanda,’’ Alisema Balozi Shelukindo.
Naye Mwenyekiti Mwenza, Balozi Selma Malika katika hotuba yake
ameeleza kuwa mkutano huu wa tano unaonesha utayari wa pande zote
mbili katika kukuza ushirikiano wenye tija kwa maslahi ya watu wake.
‘’Serikali ya Algeria itaendelea kuhuisha na kuimarisha ushirikiano na
Serikali ya Tanzania katika masuala ya diplomasia, biashara, mafunzo
ya kujenga uwezo na tafiti, ufadhili katika elimu ya juu na kuongeza
maeneo mapya ya ushirikiano kila inapohitajika ili kujenga uchumi
imara wa mataifa yetu,’’ alisema Balozi Selma Malika.
Aidha, kupitia mkutano huu Balozi Shelukindo amewasilisha salamu za
pole kwa Serikali ya Algeria kufuatia tukio la janga la moto lililotokea
katika mikoa ya Bejaia, Jijel, Bouira, Media, Skikda na Tiziozou
ulilosababishwa na kuongezeka kwa joto kali. 
Tanzania na Algeria zinashirikiana katika sekta za Biashara, viwanda,
kilimo, miundombinu, nishati, madini, utalii, sanaa na utamaduni, elimu,
sayansi na teknolojia, ulinzi na usalama, siasa na diplomasia,
mawasiliano, uvuvi, uwekezaji na maendeleo ya jamii.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *