KITAIFA

WAAJIRI WATAKIWA KUWARUHUSU MAKATIBU MUHSUSI, WATUNZA KUMBUKUMBU KUSHIRIKI MKUTANO UTAKAOWAJENGEA UWEZO

WAAJIRI WATAKIWA KUWARUHUSU MAKATIBU MUHSUSI, WATUNZA KUMBUKUMBU KUSHIRIKI MKUTANO UTAKAOWAJENGEA UWEZO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Waandishi wa Habari na Watendaji wa ofisi yake (hawapo pichani) jijini Dodoma kuhusu mkutano wa kitaaluma wa Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu utakaofanyika Zanzibar..

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka waajiri katika
Taasisi za Umma na Sekta Binafsi kuwaruhusu na kuwawezesha Makatibu
Mahsusi na Watunza Kumbukumbu kushiriki mkutano wa kitaaluma
unaotarajiwa kufanyika Zanzibar kwa lengo la kuwajengea uwezo
kiutendaji ili waweze kutimiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora kwa
Watanzania pamoja na kuleta maendeleo katika taifa.
Mhe. Simbachawene ametoa wito huo jijini Dodoma, wakati wa mkutano
wake na Waandishi wa Habari kuhusu umuhimu wa Makatibu Muhsusi na
Watunza Kumbukumbu kushiriki mkutano wa kitaaluma ambao Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
alielekeza ufanyike Zanzibar.
Mhe. Simbachawene amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha
utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi unakuwa
uliotukuka na wenye lengo la kuwahudumia wananchi, hivyo amewahimiza
waajiri kuwaruhusu Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu kushiriki
mkutano huo wa kitaaluma ili wapate ujuzi na maarifa ya kutekeleza
majukumu yao kwa ufanisi.
“Mheshimiwa Rais kwa kutambua umuhimu wa kada hizi za Makatibu
Mahsusi na Watunza Kumbukumbu katika utendaji wa shughuli za Serikali
na Sekta Binafsi, alielekeza ufanyike mkutano mkubwa wa kitaaluma
Zanzibar ili washiriki wapate fursa ya kujadili namna ya kuboresha utendaji
kazi wao wa kila siku,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.


Mhe. Simbachawene amewahimiza waajiri kuhakikisha idadi kubwa ya
Makatibu Mahususi na Watunza Kumbukumbu wanashiriki mkutano huo na
kuwagharamia, ili ushiriki wao uwe na tija kiutendaji pindi watakaporejea
katika maeneo yao ya kazi.

Sehemu ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma kuhusu mkutano wa kitaaluma wa Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu utakaofanyika Zanzibar.

Mhe. Simbachawene amesema mkutano huo utakaoongozwa na kaulimbiu
isemayo “Nidhamu, Uadilifu na Utunzaji Siri Sehemu za Kazi ni Chachu
ya Maendeleo Kitaaluma” utafunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Viwanja
vya Mao Tse Tung, Zanzibar Mkoa wa Mjini Magharibi.
Mhe. Simbachawene amesema, maandalizi ya mkutano huo unaoratibiwa
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yamekamilika kwa kiasi kubwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan, wakati wa Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Menejimenti ya
Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) uliofanyika tarehe 27/11/2022 jijini
Arusha, alielekeza ufanyike mkutano wa pamoja Zanzibar wa TAPSEA na
TRAMPA utakaowawezesha kubadilishana uzoefu kiutendaji na kuweka
mikakati endelevu na madhubuti ya kuboresha utendaji kazi wao wa kila
siku.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *