KITAIFA

WAPIGA RAMLI CHONGANISHI, NOTI BANDIA, BODABODA, SILAHA ZA JADI BUNDUKI, MIKONONI MWA POLISI SHINYANGA

WAPIGA RAMLI CHONGANISHI, NOTI BANDIA, BODABODA, SILAHA ZA JADI BUNDUKI, MIKONONI MWA POLISI SHINYANGA

KUTOKA SHINYANGA: Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa 12 na wengine wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ikiwemo kukamatwa noti bandia 15 zenye thamani ya Tsh, 150,000/=, silaha, na vifaa vya kupiga ramli chonganishi vya kufanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kibali maalum.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamis Septemba 21,2023.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Alhamisi Septemba 21,2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema watuhumiwa hao wamekatwa kupitia misako na doria iliyofanywa katika maeneo mbalimbali katika kipindi cha mwezi Agosti mpaka Septemba, 2023 ikiwa ni katika kuendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda maisha ya watu na mali zao.

Amefafanua kuwa pia wamefanikiwa kukamata Silaha aina ya Shortgun BELGIUM yenye namba 18342 ambayo ilikuwa inamilikiwa isivyo halali, Wamemekamata silaha nyingine aina ya Shortgun Pump Action yenye namba za usajili TZ CAR 69657A ambayo ilitumika katika tukio la unyang’anyi na kuitelekeza baada ya kugundua kuwa wanafuatiliwa na askari.

Kwa upande wa makosa ya usalama barabarani, amesema Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita lilifanikiwa kukamata jumla ya makosa mbalimbali 3636 ya usalama barabarani ambapo jumla ya magari yaliyokamatwa yalikuwa 2850. magari mabovu ni 1053, kuzidisha abiria ni 429, kutokuwa na Bima ni 163, kuendesha magari kwa njia hatarishi ni 139, kutofunga mikanda ya usalama ni 31, kuendesha magari bila leseni ni 05 na kuendesha magari kwa mwendokasi ni 509, makosa na mengineyo 521.

Amesema jumla ya Pikipiki na Bajaji 786 zilikamatwa kwa makosa mbalimbali ambapo Pikipiki mbovu zilikuwa ni 59, kutovaa kofia ngumu ni 182, kuzidisha abiria ni 76, kuendesha Pikipiki bila Bima ni 163, kuendesha pikipiki kwa njia hatarishi ni 33, kulewa na kuendesha pikipiki ni 01, kuendeha pikipiki bila leseni ni 203 na kutokuwa na leseni ya usafirishaji ni 69

Akielezea mafanikio yaliyofikiwa na Jeshi la Polisi katika kipindi cha Mwezi Agosti hadi Septemba 2023, Kamanda Magomi amesema mtuhumiwa 01 wa kesi ya kubaka alihukumiwa kifungo cha maisha jela na watuhumiwa wengine 04 walihukumiwa kifungo cha miaka 30 Jela kila mmoja kwa kosa hilo hilo la kubaka ambapo walitenda makosa hayo katika nyakati tofauti.

Amesema kesi za wizi zilikuwa 03 na zilihukumiwa kulipa faini kati ya Tsh. 100,000/= hadi 500,000/=, kesi 01 ya kutelekeza familia mshtakiwa alifungwa miezi 06 jela, kesi 01 ya kutorosha mwanafunzi ilihukumiwa kuchapwa viboko 05, kutupa mtoto kesi 01 ilihukumiwa miaka 02 ya kutumikia jamii, kupatikana na Bangi kesi 01 ilihukumiwa kutumikia jamii kwa kipindi cha mwezi 01 na pia kupatikana na madawa ya kulevya kesi 02 zilihukumiwa kifungo cha miaka 02 jela

Kamanda huyo wa Polisi amesema Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linaendelea kuwashukuru raia wema wote wanaotoa taarifa za uhalifu na wahalifu zinazoleta mafanikio haya na linawaasa wananchi wote kuendelea kutii sheria za nchi kuuweka mkoa wa Shinyanga kwenye hali ushwari.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *