KITAIFA

HOTUBA MAKAMU WA RAIS DKT. PHILIP MPANGO AKIFUNGUA NANENANE 2023 MBEYA

HOTUBA MAKAMU WA RAIS DKT. PHILIP MPANGO AKIFUNGUA NANENANE 2023 MBEYA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akihutubia viongozi, wadau wa sekta ya kilimo na ufugaji pamoja na
wananchi mbalimbali wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya
Nane nane leo tarehe 01 Agosti 2023 yanayofanyika katika viwanja vya John
Mwakangale mkoani Mbeya.

Ndugu Wananchi,
Kwanza, napenda kuwaletea salamu za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anawapongeza na
kuwashukuru wakulima, wafugaji na wavuvi nchini kote kwa kazi nzuri ambayo
inalihakikishia Taifa usalama wa chakula, upatikanaji wa malighafi za viwanda,
ajira, kipato na kuliingizia Taifa fedha za kigeni na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Pili, napenda kuwashukuru Waheshimiwa na taasisi zifuatazo kwa maandalizi ya
kiwango ya Nanenane 2023: Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo; Abdallah
Hamis Ulega (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi; Juma Homera, Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya; Wakuu wa Mikoa ya Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma, Rukwa na
Katavi; viongozi na watumishi wa Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya
Rais TAMISEMI, Maji, Viwanda na Biashara, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi pamoja na Kamati ya Maandalizi na Wananchi wote mliojitokeza kushiriki
Maonesho haya.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wagunduzi wa mbegu bora zenye mchango mkubwa kwenye usalama wa chakula nchini waliopewa tuzo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nane nane leo tarehe 01 Agosti 2023 yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.


Ndugu Wananchi;
Kaulimbio ya Maadhimisho haya kwa mwaka 2023 inasema “Vijana na
Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula”. Kaulimbiu
hii inalenga kutukumbusha kuthamini mchango mkubwa wa Vijana na
Wanawake katika shughuli za maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kiuhalisia,
vijana na wanawake ndiyo wanaochangia sehemu kubwa ya nguvu kazi katika
uzalishaji, uchakataji, usambazaji na uuzaji wa chakula katika masoko ya ndani
na nje ya nchi. Wanawake Oyeee!! Vijana Oyeee!!


Ndugu Wananchi;
Katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka
2020, Serikali imedhamiria kuendeleza Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili
kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
pamoja na kukuza kipato na kutoa ajira kwa wananchi. Kwa sababu hiyo,
Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Shilingi 275
bilioni mwaka 2021/2022 hadi Shilingi 295 bilioni mwaka 2023/24 na ile ya
Wizara ya Kilimo kutoka Shilingi 294,162,071,000 kwa mwaka 2021/2022
hadi Shilingi 970,785,619,000 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la
asilimia 330.02. Mama Samia Oyeee!! Mifugo Oyeeee!! Kilimo
Oyeeee!! Ongezeko hili linalenga kuimarisha maeneo mahsusi ya utafiti na
huduma za ugani; kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo, mifugo na uvuvi;
kuimarisha na kutoa huduma ya upimaji wa afya ya udongo; kuendeleza kilimo
cha umwagiliaji; kuimarisha upatikanaji wa Mitaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha
Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo; kuimarisha miundombinu ya uhifadhi wa mazao
ya kilimo; kuhamasisha na kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa ya pamoja
na kuimarisha maendeleo ya ushirika.


Ndugu Wananchi,

Mauzo ya mazao ya chakula yamekuwa chanzo cha ongezeko la fedha za kigeni
katika uchumi wa nchi yetu. Mathalan, thamani ya mauzo ya mahindi nje ya nchi
yameongezeka kutoka Dola za Marekani 57,097,279 kwa mwaka 2021 hadi
Dola 71,543,641 mwaka 2022 na thamani ya mauzo ya ufuta kutoka Dola za
Marekani 123,000,627 mwaka 2021 hadi Dola 143,788,838 mwaka 2022.
Hivyo, natoa rai kwa wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ili nchi
yetu iweze kujitosheleza kwa chakula na kupata fedha zaidi za kigeni kutokana
na mazao mbalimbali.


Ndugu Wananchi,
Katika kuongeza matumizi ya mbolea nchini, Serikali inaendelea kuimarisha
upatikanaji na kuhimiza matumizi ya mbolea kupitia Mpango wa ruzuku ili
kuongeza tija na uzalishaji. Kupitia Mpango huo matumizi ya mbolea kwa mwaka
2022/2023 yamefikia tani 580,628 ikilinganishwa na tani 363,599 kwa mwaka
2021/2022. Aidha, katika mwaka 2023/2024 Serikali itaendelea kuwezesha
upatikanaji wa mbolea nchini kupitia Mpango wa ruzuku.


Ndugu Wananchi;
Kwa kutambua mchango wa vijana na umuhimu wa kuongeza fursa za ajira,
Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimeanzisha mradi wa Jenga
Kesho Iliyo bora (Building a Better Tomorrow – BBT). Katika mradi huu (kwa
upande wa Wizara ya Kilimo) kuna vituo Atamizi 13 ambapo vijana 812
(wanawake 282 na wanaume 530) wameanza mafunzo ya kilimo biashara.
Aidha, kwa upande wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi jumla ya vituo atamizi nane
(8) vyenye jumla ya vijana 238 (71 Wanawake na 167 Wanaume) wanaendelea
na mafunzo ya unenepeshaji wa mifugo. Lengo la vituo hivi ni kuwawezesha
vijana kupata uzoefu katika kuanzisha na kuendesha miradi ya kilimo na ufugaji
kibiashara pamoja na kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mazao bora
ya mifugo, malighafi kwa ajili ya viwanda nchini na kuongeza fursa za kujiajiri.


Ndugu Wananchi;
Serikali yetu inaendelea kutoa programu ya mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji
viumbe maji kwa vijana kwa kushirikiana na Sekta binafsi ambapo jumla ya
vijana 200 (74 wanawake na 126 wanaume) wamepatiwa mafunzo haya na
mpango wa Serikali ni kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana 750. Aidha, kwa
dhati kabisa namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wetu kwa uamuzi wake wa kutoa msukumo katika uwezeshaji wa
vijana kupata ajira kupitia miradi ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better
Tomorrow – BBT), kwa upande wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Hivyo, nawasihi
vijana kuchangamkia fursa hizi ili kujipatia ajira na kukuza uchumi wao binafsi na
wa Taifa kwa ujumla. Aidha, nazielekeza Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi

kuona namna bora ya kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
ili vijana wa JKT wanaojitolea wapewe kipaumbele kushiriki katika programu hii.


Ndugu Wananchi;
Eneo lingine muhimu ni huduma za ugani ambazo ni kiungo muhimu katika
kuwezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kuongeza uzalishaji na tija. Katika
hotuba yangu ya ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane ya mwaka 2022 katika
viwanja hivi, nilisisitiza kuhusu wajibu wa Maafisa Ugani kupeleka huduma zao
kwa wakulima/wafugaji badala ya kusubiri kufuatwa. Hata hivyo, licha ya
changamoto kadhaa zinazoathiri utoaji wa huduma za ugani nchini, naendelea
kusisitiza kuhusu kuongeza kasi ya utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima
wetu. Serikali kwa upande wake itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za
ugani kwa kuwapatia Maafisa Ugani vitendea kazi mbalimbali vikiwemo pikipiki,
vifaa vya matibabu, uhimilishaji na vifaa vya kupima afya ya udongo. Aidha,
ninaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri
kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa
ikiwemo kuwapatia mafuta na kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya
pikipiki hizo.


Ndugu Wananchi;
Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji nchini ikiwemo
kujenga mabwawa ya kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya umwagiliaji, ambapo
lengo ni kufikia eneo la umwagiliaji la hekta 1,200,000 ifikapo mwaka 2025.
Hadi sasa, Serikali imefikia asilimia 60.6 sawa na hekta 727,280.6 za eneo
linalomwagiliwa. Wito wa Serikali kwa wananchi ni kutumia na kutunza
miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kusaidia kuleta tija.


Ndugu Wananchi;
Kwa kutambua umuhimu wa ushirika katika kuwaweka wakulima pamoja,
Serikali inaendelea kuhamasisha Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kujiunga na
Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) vitakavyokuwa chanzo cha
mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao na kuimarisha uwekezaji katika
kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na
uvuvi. Aidha, ili kuimarisha upatikanaji wa mitaji, Serikali inaendelea
kuhamasisha na kuzitaka taasisi za fedha kubuni bidhaa/huduma
zitakazowawezesha wananchi wengi kukopa ili kukuza mitaji yao. Natumia fursa
hii kupongeza mabenki ambayo yameanza kutekeleza jukumu hili na nazisisitiza
taasisi zote za fedha kuendelea kupunguza riba ili wakulima, wafugaji, wavuvi,
wasindikaji, wanunuzi na wajenzi wa viwanda waweze kukopa. Aidha, Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) iongeze kasi ya kutoa mikopo kwa
wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo.


Ndugu Wananchi;

Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa ambayo inaathiri shughuli za
uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Hali hii inachangiwa na shughuli
za binadamu ikiwa ni pamoja na kilimo kisichozingatia uhifadhi wa mazingira,
ufugaji usiozingatia ukubwa wa eneo, ufugaji wa kuhamahama, uvuvi haramu,
ufugaji wa viumbe maji katika maeneo yasiyoidhinishwa kisheria, ukataji wa miti
hovyo na uharibifu wa vyanzo vya maji. Katika suala hili, nawahimiza wakulima,
wafugaji, wavuvi na wananchi wote kuwa mstari wa mbele kutunza mazingira,
kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti, kufuga mifugo kulingana na ukubwa wa
eneo, kulima malisho ya mifugo yenu na kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia
za kilimo, mifugo na uvuvi zinazohimili mabadiliko ya tabia nchi.


Ndugu Wananchi;
Kabla ya kuhitimisha hotuba hii, ninapenda kuwafahamisha kuwa nchi yetu
itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika
kwa mwaka 2023 (African Food Systems Forum), utakaofanyika kuanzia tarehe 5
hadi 8 Septemba, 2023 Jijini Dar es Salaam. Hii ni heshima kwa nchi yetu na
fursa ya kuvutia uwekezaji katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Nawahimiza
wadau wote wa sekta hizi hususan sekta binafsi kuchangamkia fursa ya kushiriki
katika jukwaa hilo litakalokuwa na washiriki wasiopungua 3,000 kutoka nchi
mbalimbali.


Ndugu Wananchi;
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kutoa msisitizo wa masuala muhimu
yafuatayo:
Jambo la Kwanza, makundi makubwa ya mifugo yameingizwa katika mikoa ya
nyanda za juu kusini! Madhara yake ni makubwa sana, ikiwemo kuharibiwa sana
kwa mazingira. Aidha, imezuka migororo mingi kati ya wakulima na wafugaji.
Migororo hii imepelekea uharibifu wa mazao, mifugo na binadamu kuuawa au
kujeruhiwa. Wanyama kama Tembo nao wanakimbia bugudha ya mifugo na sasa
wanahamia kwenye makazi ya binadamu wakiharibu mazao na hata kuua watu.
Hivyo, Wizara zote husika na Wakuu wa Mikoa wachukue hatua thabiti kudhibiti
uingizaji mifugo kinyemela katika maeneo yao ya utawala. Aidha, watenge na
kupima vitalu/mashamba ya mifugo na kushirikiana na wamiliki wa mifugo
kujenga malambo na kuendeleza malisho na pia kuuza mifugo ya ziada.
Jambo la Pili, matumizi sahihi ya viuatilifu na kemikali. Kumekuwepo matumizi
yasiyo sahihi ya viuatilifu na kemikali nyingine. Jambo hili lina athari kubwa kwa
afya ya binadamu na viumbe hai vingine. Nawasihi wakulima, wafugaji na
wavuvi kuzingatia maelekezo ya wataalam ili tuweze kuzalisha pasipo kuathiri
afya ya binadamu na mazingira yetu.

Jambo la Tatu, kuenea kwa mtindo wa kubadili matumizi ya ardhi iliyotengwa
mahsusi kwa ajili ya Utafiti Kilimo. Maeneo mengi ya taasisi za utafiti
yamevamiwa na kupimwa viwanja! Jambo ambalo linatishia utafiti wa kilimo na
mifugo kwa kuwa vituo vyetu vya utafiti vitakosa maeneo ya kutosha ya kufanyia
kazi. Ndugu zangu Watanzania lazima tutambue kuwa kilimo ni Sayansi na
Utafiti Kilimo usipopewa kipaumbele basi mapinduzi ya kilimo yatabaki kuwa
ndoto. Hivyo, maeneo ya taasisi za Utafiti Kilimo yapimwe, yapewe hati miliki na
yalindwe. Vivyo hivyo, kuna uhaba wa maeneo mahsusi ya kuzalishia mbegu. Hii
inatokana na kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa kutenga maeneo kwa
madhumuni ya uzalishaji wa mbegu na pia utunzaji wa yale yaliyopo. Kwa kuwa
maeneo ya uzalishaji wa mbegu si kama maeneo ya kilimo cha mazao ya
kawaida, naelekeza Mamlaka zinazohusika pia kutenga na kupima ardhi kwa ajili
ya madhumuni hayo na kuyalinda dhidi ya uvamizi.
Jambo la Nne, usalama wa chakula katika kaya. Nasisitiza wananchi kutouza
chakula chote na badala yake kuhifadhi chakula kwa ajili ya matumizi ya kaya.
Kuhakikisha usalama wa chakula katika kaya uwe wajibu wa msingi wa kila kaya
nchini. Aidha, kwa mazao ya kibiashara nawasihi wakulima kutoyauza kabla ya
kukomaa na kufikia ubora unaokubalika. Hii ni muhimu ili kutoharibu soko la
mazao yetu ndani na nje ya nchi. Naelekeza Wizara ya Kilimo kuweka utaratibu
mzuri wa kuhakiki ubora wa mbegu zinazouzwa na mazao.
Jambo la Tano, ni tatizo la uhaba wa mbegu za malisho na mbegu bora za
mifugo vikiwemo vifaranga vya Samaki. Tatizo hili linakwamisha juhudi za
kukuza na kupanua kilimo na ufugaji kwa kiasi kikubwa. Naelekeza Wizara
husika na taasisi za utafiti wa mifugo na viumbe maji kuhakikisha mbegu za
malisho na mifugo zinapatikana kwa wananchi na kwa gharama nafuu.


Ndugu Wananchi,
Nimefarijika na nimeridhika na kiwango cha maandalizi ya maonesho haya.
Nawahimiza wananchi wa Jiji la Mbeya na Mkoa mzima waje kutembelea
maonesho haya, wajifunze na kujionea bidhaa mbalimbali za kilimo na mifugo
lakini pia fursa nyingi zilizoko katika sekta hizi kwa ajili ya maendeleo yao na
Taifa letu.
Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa Maonesho na sherehe za
Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kwa mwaka 2023
yamefunguliwa rasmi.

Asanteni kwa kunisikiliza

About Author

Bongo News

2 Comments

    esse quos omnis et dolore repellat dignissimos. ad modi quaerat consequatur recusandae sapiente odit commodi.

    ut non et eos eaque saepe maxime expedita libero ratione quas modi aut et ducimus sit quasi dignissimos. et voluptatem qui occaecati dolorem ab quo. aliquam totam iusto nulla voluptas maiores commodi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *