Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imetoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna Nchini ya Tanzania inavyokuza na kulinda Haki za Kiraia, Kisiasa, Kiuchumi, Kiutamaduni na Kijamii.

Hayo yamewekwa bayana na Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo Prof.Lemy Ngoy Lumbu katika Kikao cha 83 cha Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, kinachofanyika katika makao makuu ya Kamisheni hiyo jijini Banjul Gambia ambapo Tanzania inawakilishwa na Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Idara ya Haki za Binadamu.
Akiwasilisha taarifa ya Tanzania Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Candid Nasua amewaeleza Wanachama wa kikao hicho kuhusu falsafa ya Rais Samia katika kuhakikisha Haki za Binadamu hazikiukwi ikiwa ni pamoja na Maridhiano, Ustahimilivu ,Mageuzi na Kujenga Upya Taifa ambapo kwa kupitia majadiliano na ushirikiano imechangia katika kuimarisha Haki za Binadamu, umoja wa Kitaifa, Amani pamoja na kuleta maendeleo Nchini.

Nasua ameeleza kuwa kwa kuzingatia Haki za Kiraia na Kisiasa, mwaka huu Nchi ya Tanzania inatarajia kuwa na Uchaguzi Mkuu na kwa mwaka 2024 Tanzania ilifanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo vyama vya siasa vyenye usajili viliweza kushiriki.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuhakikisha watu wanufaika na Uhuru wa kujieleza na Haki ya kupata taarifa.
Pia Nasua ameongeza kuwa katika kusimamia Haki za wenye Ulemavu Serikali ya Tanzania ilizindua Mpango wa Kazi wa Kitaifa wa Haki na Ustawi wa Watu wenye Ualbino pamoja na mkakati wa Teknolojia ya kuwasaidia watu wenye Ulemavu inalindwa ikienda sambamba na usogezaji wa huduma mbalimbali karibu na Wananchi kama vile maji,umeme na huduma za afya.)

Nasua ameongeza kuwa Serikali imeendelea kushirikiana na asasi za Kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo katika nyanja mbalimbali.