KITAIFA

MANYARA KUTIBU WAGONJWA ELFU 11 WENYE SHINIKIZO LA DAMU KILA MWAKA

MANYARA KUTIBU WAGONJWA ELFU 11 WENYE SHINIKIZO LA DAMU KILA MWAKA

Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) Dkt. Yesige Mutajwaa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete baada ya maadhimisho ya siku ya shinikizo la juu la damu yaliyofanyika kitaifa leo Mkoani Manyara. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Pima shinikizo lako la damu kwa usahihi, lidhibiti ili uishi maisha marefu”.

Wagonjwa elfu 11 wenye tatizo la shinikizo la juu la damu hupata
matibabu ya ugonjwa huo kila mwaka katika vituo vya afya vilivyopo Mkoa wa
Manyara.
Hayo yamesemwa na mgeni rasmi wa maadhimisho ya siku ya Shinikizo la juu la
damu Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara Dkt. Yesige
Mutajwaa wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika Kitaifa leo Mkoani
Manyara.
Dkt. Yesige ambaye pia daktari bingwa wa magonjwa ya ndani alisema idadi hiyo
sio idadi kamili ya watu wenye shinikizo la juu la damu kwani hao elfu 11 ni idadi
ya wale tu wanaopata matibabu katika Mkoa huo.
“Tangu mwaka 2018 hadi 2022 mwelekeo wa shinikizo la juu la damu kwa
wananchi wa Manyara unaonyesha kuongezeka, mwaka 2018 wananchi wote
walioudhuria vituo vya kutolea huduma za afya asilimia 0.9 walikutwa na shinikizo
la juu la damu ambalo kila mwaka limekuwa likiongezeka hivyo mwaka 2022
wagonjwa wa shikikizo la juu la damu walioudhuria vituo vya afya Manyara kufikia
asilimia 1.4”, alisema Dkt. Yesige.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo akielezea namna ambavyo JKCI imekuwa ikiwafikia
wagonjwa wa shinikizo la damu katika mikoa mbalimbali wakati wa maadhimisho
ya siku ya shinikizo la juu la damu yaliyofanyika kitaifa leo Mkoani Manyara. Kauli
mbiu ya mwaka huu ni “Pima shinikizo lako la damu kwa usahihi, lidhibiti ili uishi
maisha marefu”.

Dkt. Yesige alisema kumekuwa na changamoto ya uhaba wa dawa katika vituo vya
kutolea huduma za afya, lakini wao kama Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara
wamejipanga na kuwapa uwezo wataalam weo kuweza kufanya maoteo vizuri ya
dawa ili wananchi wanapofika katika Hospitali hiyo wasikutane na changamoto
dawa.
Aidha Dkt. Yesige ameishukuru Wizara ya Afya kwa kukubali na kuuchagua mkoa
wa Manyara kuwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya shinikizo la juu la damu
kitaifa kwani kupitia maadhimisho hayo kunatoa hamasa kwa wananchi wa
Manyara kuona umuhimu wa kupima shinikizo la juu la damu mara kwa mara.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo alisema JKCI ilianzisha kambi maalum za
matibabu ya moyo lengo likiwa kusogeza huduma karibu na wananchi,

kujengeana uwezo watumishi wa afya, pamoja na kuielimisha jamii juu ya
magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt. Pedro alisema magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu
yameongezeka katika jamii hivyo ni wakati muafaka kama wadau wa afya kupigia
kelele kuipa hamasa jamii kuhusu uelewa wa magonjwa hayo ili kwa pamoja jamii
iweze kujikinga.
“Hadi sasa JKCI imeshatoa huduma na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza
katika mikoa 10 ikiwemo mkoa wa Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Iringa,
Dodoma, Dar es Salaam, Pwani, na Manyara”,
“Kupitia kambi maalum za matibabu ya moyo tulizoziendesha tumeshatoa
huduma za upimaji wa shinikizo la juu la damu pamoja na moyo kwa watu zaidi ya
elfu 8 ambapo katika maeneo yote tuliyopita ugonjwa wa shinikizo la juu la damu
ndio ulioongoza katika magonjwa yote ambayo tumeweza kuyatambua”, alisema
Dkt. Pedro
Kwa upande wa huduma zinazotolewa JKCI Dkt. Pedro alisema kila wagonjwa 7
kati ya 10 wanaofika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya huduma tatizo
wanalokutwa nalo ni shinikizo la juu la damu, na matokeo hayo pia huonekana
katika jamii kwani katika kambi wanazozifanya kati ya wagonjwa 4 kati ya 10
hukutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.
Naye Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukiza Wizara ya Afya Anzibert Rugakingira
alisema Wizara ya afya yenye jukumu la kulinda afya za wanzania ipo mstari wa
mbele kuhakikisha wananchi wanajua namba zao za shinikizo la juu la damu
kujitambua na kupatiwa matibabu mapema.

Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH)
Dkt. Yesige Mutajwaa akikata utepe kuashiria maadhimisho ya siku ya shinikizo la
juu la damu huku pembeni yake daktari bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo akimpima shinikizo la damu Mratibu wa
magonjwa yasiyoambukiza Wizara ya Afya Dkt. Anzibert Rugakingira wakati wa
maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa leo katika Mkoa wa Manyara


Dkt. Rugakingira alisema nimuhimu kila mtu akawa na utaratibu ya kupia shinikizo
la juu la damu angalau mara mbili kwa mwaka ili pale mtu anapokuwa na tatizo
hilo aweze kupata matibabu kwa haraka kupunguza athari anazoweza kupata
kama hatatibiwa mapema.

Dkt. Rugakingira alisema Wizara ya Afya inao mpango wa taifa wa kuzuia na
kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, mpango huo ulianzishwa baada ya kuwepo
na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza hapa nchini.
“Kwa muda wa kipindi cha miaka mitano utafiti umefanyika ambapo 2017
wagonjwa wa shinikizo la juu la damu walioudhuria vituo vya afya walikuwa laki
sita na elfu themanini na nane, 2022 wagonjwa hao waliongezeka hadi kufikia
milioni moja na laki nne, wagonjwa hawa ni wale tu wanaoudhuria kliniki naamini
wapo wagonjwa wengi ambao upoteza maisha yao bila ya kufika Hospitali kupata
huduma” alisema Dkt. Rugakingira

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *