KITAIFA

MSONGO WA MAWAZO WATAJWA KUWA SABABU YA KUATHIRI AFYA YA WAJAWAZITO NA LISHE KWA WATOTO

MSONGO WA MAWAZO WATAJWA KUWA SABABU YA KUATHIRI AFYA YA WAJAWAZITO NA LISHE KWA WATOTO

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akifungua maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa  ya mama kwa mtoto  mbele ya  waandishi wa habari (hawapo pichani) iliyoanza tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2023 yenye kauli mbiu isemayo”Saidia Unyonyeshaji: Wezesha Wazazi Kulea Watoto na  Kufanya Kazi zao Kila Siku”.

Wajawazito nchini wametakiwa kukaa katika mazingira yasiyowaletea msongo wa mawazo katika kipindi chote cha ujauzito na unyonyeshaji ili kufanya maziwa yatoke vizuri na mtoto kupata lishe bora na kukua vizuri 

Wito huo umetolewa leo na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati wa uzinduzi wa wiki ya unyonyeshaji inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 8 kwenye ukumbi wa ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mollel amesema kuwa, mama mjamzito anahitaji matunzo kwaajili ya lishe ya mtoto katika siku 1000 Yaani tangu kutungwa kwa mimba hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili kwani ndio msingi bora wa ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili.

“Katika siku hizi 1000 madhara ya lishe duni hasa udumavu yanaathiri sana maendeleo ya rasilimali watu ya nchi, hivyo ni muhimu mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo na kuendelea kunyonyeshwa huku akipatiwa chakula cha nyongeza hadi anapotimiza miaka miwili au zaidi.” Amesema Dkt. Mollel

Aidha, Dkt. Mollel amesema, watoto wadogo na watu wazima wanapaswa kula lishe bora ili kuwaepusha na magonjwa yanayotokana na kutokula lishe isiyokamilika.

Picha ya pamoja ya wataalamu wa lishe kutoka Wizara ya Afya pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) mara baada ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya unyonyeshaji  maziwa ya mama kwa mtoto

“Kuna magonjwa mengi yanayotokana na kutokula lishe kamili ni vyema watoto na watu wazima kuzingatia hilo, pia lishe inayozidi inasababisha uzito uliozidi na hivyo kusababisha magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Figo na moyo.”Alisisitiza Dkt. Mollel

Kuhusu takwimu za lishe Naibu Waziri alisema, asilimia ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee imeongezeka kutoka 58% mwaka 2018 hadi kufikia 64% mwaka 2022.

Vile vile takwimu ya watoto wanaonyonyeshwa ndani ya saa 1 baada ya kuzaliwa imeongezeka kutoka 53.5% mwaka 2018 hadi kufikia 70% mwaka 2022.

Hata hivyo Dkt. Mollel amewahimiza waajiri katika Sekta rasmi na zisizo rasmi na jamii kwa ujumla kuwasaidia wanawake waweze kunyonyesha watoto wao huku wakiendelea kufanya kazi na kuwakumbusha viongozi, wasimamizi, Wataalamu na watendaji kuendelea  kuelimisha umma kuhusu sheria ya kulinda haki za uzazi kwa wanawake pamoja na kuwahimiza waajiri kutenga sehemu maalum kwa ajili ya wafanyakazi wanawake wanaonyonyesha ili waweze kuendelea kufanya hivyo wakiwa kazini.

Naye Mwakilishi wa wadau wa Lishe nchini kutoka UNICEF Bw. Patrick Codjia ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa dhamira ya dhati ya kuboresha lishe, afya na maisha ya wananchi wake ikiwa ni pamoja na watoto.

Wakati huo huo Mwakilishi kutoka Shirika la Kimatifa la Kazi(ILO) Bi. Chiku Semfuko ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa muda kwa wanawake kwenda kunyonyesha pia kutenga vyumba maalumu vya kunyonyesha ili kuwapa nafasi wanaonyonyesha.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *