KITAIFA

NEC YATANGAZA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA MBARALI

NEC YATANGAZA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA MBARALI

Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw.Ramadhani Kailima 

Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara utafanyika
tarehe 19 Septemba, 2023.
Akisoma taarifa kwa umma jijini Dodoma leo tarehe 05 Agosti, 2023, Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima amesema
wagombea watachukua fomu kuanzia tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023, siku ya uteuzi
itakuwa tarehe 19 Agosti, 2023 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe
20 Agosti, 2023 hadi tarehe 18 Septemba, 2023.
Amezitaja kata zitakazofanya uchaguzi mdogo kuwa ni; Nala iliyopo Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya
Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya
Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani
Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki
iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.
“Tume inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau
wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu,
Miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huu mdogo,”
amesema Bw. Kailima.
Aliongeza kuwa, Tume imetoa taarifa hiyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiitaarifu Tume kuhusu
uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Mbarali, Halmashauri ya Wilaya ya
Mbarali Mkoa wa Mbeya. Nafasi hiyo wazi inatokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge
wa Jimbo hilo, Mhe. Francis Mtega. Spika ametoa taarifa hiyo kwa mujibu wa
kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
“Tume imepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye Dhamana ya Serikali za Mitaa,
akiitarifu juu ya uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika kata sita za Tanzania
Bara. Waziri ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(1) cha
Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292,” alisema Bw. Kailima.
Aliongeza, “Tume kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37(1)(b) cha Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya
Serikali za Mitaa, Sura ya 292 inatoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi
mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Mbarali na Madiwani katika kata sita za Tanzania
Bara”.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *