KITAIFA

NYANGASA: KISARAWE JITOKEZENI KUPIMA MOYO

NYANGASA: KISARAWE JITOKEZENI KUPIMA MOYO

Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Mhe.Fatma Nyangasa akizungumza na wananchi waliofika katika Hospitali ya wilaya hiyo kwajili ya kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya siku tatu ya matibabu inayofanyika wilayani humo.

Wananchi wa Kisarawe na wilaya jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za upimaji, ushauri  na matibabu ya moyo zinatotolewa na watalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya wilaya Kisarawe.

Wito huo umetolewa jana na  Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Mhe.Fatma Nyangasa wakati akifungua kambi maalumu ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanyika katika Hospitali ya wilaya Kisarawe.

Mhe. Fatma alisema  kuwepo kwa kambi hiyo  ya matibabu kunatekeleza azma ya Rais wa awamu ya sita Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo.

 “Wananchi wa Kisarawe mjitokeze kwa wingi kuchuguza afya zenu endapo mtagundulika kuwa na maradhi ya moyo mtapatiwa tiba hapa hapa Kisarawe kwani tumejipanga kuwahudumia  na hii siyo kwa Kisarawe peke yake bali na maeneo ya jirani”.

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya  (JKCI) Lisa Mageta akizungumza na diwani wa viti maalumu wa tarafa ya Sumn’gwi wilaya Kisarawe Valeriana Mkoka aliyefika katika hospitali ya wilaya Kisarawe  kwaajili ya kupata  huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayotolewa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Kisarawe.

“Kwa kushirikiana na wenzetu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tumesogeza huduma kwa wananchi wetu wa Kisarawe kwa kufanya upimaji na matibabu ya moyo. Wataalamu hawa wapo hapa kwaajili ya kutoa huduma hii,na huu ni mwendelezo wa kupatikana kwa huduma nyingine za kibigwa  katika hospitali hii ya wilaya kwani vifaa tiba vipo, dawa zipo za kutosha, wataalamu wapo uko tayari kuwahudumia wananchi wote”,alisema Mhe.Fatma.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Baraka Ndelwa alisema wapo Kisarawe kwaajili ya kutoa huduma za kibingwa za upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wote wa Kisarawe pamoja na wilaya jirani.

Dkt. Ndelwa alisema licha ya kutoa huduma ya upimaji na matibabu ya moyo wanatoa pia elimu kwa wananchi ya kujikinga na magojwa hayo na jinsi ya kutumia dawa kwa usahihi kwa wale ambao ni wagonjwa wa moyo.

 Wananchi wa wilaya ya Kisarawe wakisubiri kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya  (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya wilaya Kisarawe wakati wa kambi maalum ya siku tatu ya matibabu inayofanyika wilayani humo.

 “Tumekuja katika hospitali ya wilaya ya Kisarawe kwaajili ya kutoa huduma bobezi kwa wananchi na kuwapa elimu ya mtindo bora wa maisha ili wajikinge na maradhi ya moyo kwani maradhi haya yanazidi kuongezeka kwa sababu jamii haina elimu ya kutosha ya jinsi ya kujikinga  na maradhi ya moyo”,alisema Dkt. Ndelwa.

Naye mganga mkuu wa Kisarawe Dkt. Zaituni Hamza alisema hiyo ni  kambi ya kwanza ya matibabu ya magojwa ya moyo kufanyika  katika hospitali ya wilaya na wanategemea kuwahudumia wananchi wote wa Kisarawe na maeneo ya jirani.

Dkt. Zaituni alisema  wataalamu hao watatoa huduma za kimatibabu pamoja na uchunguzi wa kina wa  moyo kwa kutumia machine ya kuuchunguza moyo namna unavyofanya kazi (Echocardiograph).

Akizungumzia uwepo wa kliniki ya magonjwa ya moyo Dkt. Zaituni alisema mara baada ya kumalizika kwa kambi hiyo madaktari wa magonjwa ya moyo wa (JKCI) wataendelea kuwaona wagonjwa wa moyo katika hospitali ya Kisarawe.

“Kumalizika kwa kambi hii ya matibabu sio mwisho wa kutolewa kwa huduma hizi za magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Kisarawe,huduma hii itaendelea kutolewa na madaktari wa (JKCI)  kwa wananchi kwa utaratibu tutakaouweka”.

Wananchi waliopata huduma ya uchunguzi na matibabu katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kuiomba Serikali iwe inaitoa mara kwa mara kwani inawasaidia  kupata huduma kwa urahisi zaido tofauti na kama wangeifuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam.

Ahmadi Nguyu mkazi wa Kilombero mkoani Morogoro alisema katika kambi hiyo amepata huduma nzuri ya uchunguzi, ushauri  na kupewa dawa za kutosha za kwenda kutumia.

‘’Baada ya kufanyiwa uchunguzi nimegundulika nina tatizo la shinikizo la juu la damu nimepewa dawa za kutumia,nashukuru kwa huduma niliyoipata ninaomba huduma hii iendelee kutolewa na sehemu nyingine ili wananchi wote waweze kufaidika nayo”, .alisema Ahmadi.

Mwisho

About Author

Bongo News

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *