KITAIFA

WAZIRI MABULA ATAKA WAMILIKI WA ARDHI KULIPA KODI KWA WAKATI

WAZIRI MABULA ATAKA WAMILIKI WA ARDHI KULIPA KODI KWA WAKATI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi hati milki sita za ardhi mkazi wa Ngara mkoani Kagera Godfrey Niyonzima wakati wa ziara yake mkoani humo.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wamiliki wa ardhi nchini kuhakikisha wanalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati ili kuepuka kutozwa riba ya malimbikizo ya kodi hiyo.

Dkt Mabula alisema hayo wilayani Ngara mkoa wa Kagera wakati akikabidhi hati miliki za ardhi kwa wananchi wa wilaya hiyo wakati wa ziara yake mkoani Kagera.

Aliwataka wamiliki wa ardhi nchini wanaopatiwa hati milki kuendelea kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka na kubainisha kuwa, iwapo mmiliki atapitisha mwaka mmoja bila kulipa kodi basi atalazimika kulipa kodi inayoambatana na riba.

‘’kila mwaka wewe kalipe ili uwe mteja mzuri wa serikali, katika ardhi uliyo nayo usilimbilize madeni maana mwisho wa siku utakuja kushindwa na kuanza kushitakiana na serikali kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya bila sababu’’ alisema Dkt Mabula.

Dkt Mabula aliongeza kwa kusema kuwa, wizara yake imeboresha huduma zake kutoka analogia kwenda digitali unaowezesha taarifa za wamiliki wa ardhi kuwa katika mfumo wa kieletroniki na kurahisisha taratibu za utoaji hati.

‘’kwa sasa utendaji wa wizara umebadilika sana ambapo mmiliki wa ardhi anayeomba kumilikishwa anaweza kupata hati ndani ya muda mfupi iwapo atakuwa amekabilisha taratibu zote za umiliki’’. Alisema Dkt Mabula

‘’Kwetu sisi huku ambapo mifumo ya kidigitali haijakaa sawa mwombaji hati anaweza kuchukua mwezi moja ama miwili lakini kwa kule ambapo mifumo ya kidigitali ishaanza kutumika basi inaweza kabisa kuchukua hati ndani ya wiki moja’’ alisema Dkt Mabula.

Vile vile, Waziri wa Ardhi alisema kuwa, kupitia maboredsho ya huduma za sekta ya ardhi hivi sasa wamiliki wa ardhi wanapokea bili za kodi ya pango la ardhi kupitia simu zao za mkononi.

Wananchi waliopokea hati zao wameipongeza wizara ya ardhi kwa kufanya maboresho yatakayosaidia wamiliki wa ardhi kupata hati kwa muda mfupi sambamba na kupata bili za kodi kupitia simu zao za mkononi.

Mkazi wa Ngara   Godfrey Niyonzima ameshukuru kwa kupatiwa hati na kukabidhiwa na Waziri mwenye dhamana ya Ardhi hasa baada ya kuzihangaikia kuzipata hati hizo kwa takriban miaka sita.

‘’kwanza nishukuru kwa kufanikisha kupata hati zangu sita za ardhi lakini pia niipongeze wizara ya ardhi kwa kufanya maboresho ambayo naweza kusema yanakwenda kurahisisha upatikanaji hati pamoja ulipaji kodi ya pango la ardhi’’ alisema Niyonzima.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemaliza ziara yake mkoani Kagera na anatarajia kuendelea na ziara zake katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Njombe, Iringa na Morogoro.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *