KITAIFA

DED MOSHI AELEKEZWA KUMCHUKULIA HATUA MHANDISI HALMASHAURI KWA KUSHINDWA KUTIMIZA MAJUKUMU YAKE

DED MOSHI AELEKEZWA KUMCHUKULIA HATUA MHANDISI HALMASHAURI KWA KUSHINDWA KUTIMIZA MAJUKUMU YAKE

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi (aliyeinama) akijiridhisha na ubora wa sakafu katika darasa lililojengwa kwenye Shule ya Msingi Mandela iliyopo Manispaa ya Moshi, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua Ujenzi wa Miundombinu ya Elimu inayojengwa na Serikali kupitia mradi wa BOOST na SEQUIP

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.
Deogratius Ndejembi amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Moshi Bw. Shadrack Mhagama kumchukulia hatua za
kinidhamu Mhandisi Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Bw. Daniel
Kileo kwa kushindwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya elimu
ikiwemo ujenzi wa madarasa ya mradi wa BOOST kinyume na maelekezo
ya Serikali yaliyotolewa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo, mara baada ya kutoridhishwa na
ujenzi wa madarasa akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua Ujenzi
wa Miundombinu ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi
inayojengwa na Serikali kupitia mradi wa BOOST na SEQUIP.
Mhe. Ndejembi amesema, haiwezekani Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atafute fedha za kujenga
miundombinu ya elimu alafu zisitumike vizuri kwa sababu ya Mhandisi wa
Wilaya kushindwa kutafsiri ramani wakati yeye ndiye mtalaam na mwenye
jukumu hilo.
“Mkurugenzi mchukulie hatua za kinidhamu Mhandisi wa Ujenzi na
mkaimishe mwingine kwani huyu ameshindwa kusimamia ujenzi wa
madarasa na Ofisi ya Rais TAMISEMI itakuletea Mhandisi mwingine
atakayesimamia miradi ya ujenzi ya miundombinu ya elimu,” Mhe.
Ndejembi amesisitiza.
Baada ya ukaguzi wa Miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya
Moshi, Mhe. Ndejembi amebaini kuwa miradi mingi katika Halmashauri
hiyo haijakamilika wakati katika Wilaya nyingine ikiwemo Manispaa ya
Moshi imeshakamilika na changamoto kubwa kwa Halmashauri ya Wilaya
ya Moshi ikiwa ni kuwa na Mhandisi ambaye ameonekana kushindwa
kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Aidha, Mhe. Ndejembi amesema amepewa taarifa kuwa katika shule ya
Sekondari Ashira bweni moja halijajengwa licha ya kuwa fedha zilitolewa
na Serikali na Mhandishi huyo kushindwa kusimamia ujenzi huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Kisare Makori
amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa
miundombinu ya elimu na kuhimiza uwajibikaji katika Wilaya yake ili miradi
yote ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa
na Serikali.
Sanjari na hilo, Mhe. Makori amuomba Mhe. Ndejembe kumfikishia salamu
za shukrani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha
nyingi wilaya yake kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo katika sekta ya elimu, afya na miundombinu ya barabara.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *