MICHEZO

WANACHUO MALYA MABINGWA NETIBOLI

WANACHUO MALYA MABINGWA NETIBOLI

Mashindano ya Netiboli yaliyokuwa yanafanyika Kwimba mkoani Mwanza katika viunga vya
Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya yamefikia ukingoni na washinfdi kukabidhiwa zawadi
zao usiku wa Mei 22, 2023 na Makamu Mkuu wa Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya Alex
Mkenyenge.

“Hongereni kwa kushiriki mashindano haya na walioshinda nawapa
pongezi tele na ndiyo maana tunawakabidhi zawadi zenu leo hii.”

Awali jioni ya Mei 22 mashindano hayo yalianza kwa mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu
ambapo uliwakutanisha Shule ya Sekondari Nyabubinza na Wanachuo cha Malya wa ngazi ya
Astashahada, hadi robo zote nne za dakika 15 ambayo ni saa nzima za mchezo huu, wanachuo
wa Astashahada walikuwa wameshinda magoli 32 kwa 22.
Mara baada ya mshindi watatu kupatikana, uliwadia wakati wa mbwembe na majigambo
kuelekea kuanza kwa fainali iliyowakutanisha Malya Queens na Wanachuo wa Stashahada
ambapo pia katika ngazi ya makundi wanachuo wa Stashahada wa chuo hiki waliwachabanga
bila huruma wenyeji wao Malya Queens.
Mechi hiyo ushindani ulikuwa mkubwa sana huku ikitoa picha na uwezo wa Malya Quees
iliyokuwa inaongozwa na mwalimu ambaye alisoma Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya
miaka ya nyuma.
Mechi hiyo iliibua kiwewe kwa timu zote mbili ambazo sasa zilikutana fainali hiyo ya Netiboli, je
hali ingekuwaje? Hapo ndipo vituko na visa vya hapa na pale viliupamba uwanja wa ndani wa
chuo hiki cha umma huku meza ya Mgeni Rasmi ikipambwa na zawadi kadhaa zilizosindikizwa
na sauti ya mbuzi ambaye alilia meee… meee . meee… kila mara nao mashabiki wa pande zote
wakishangilia.
Walionekana mashabika hao wakifanya vituko kana kwamba wanafanya ulozi huku mashabiki
wa Malya Queens ambapo waliongezewa nguvu na wanafunzi Nyabubinza Sekondari waliovalia
sare zao za mashati meupe na sketi na suruali za rangi ya mgombamara baada ya kufungwa na
wanachuo wa Astashahada na kuikosa nafasi ya tatu.
Mashabiki wa timu ya wanachuo wa Stashahada ya Michezo kutoka Chuo cha Maendeleo ya
Michezo Malya walionekana wakiwa wamevalia nguo za kuchekesha wengine wakiwa wamevaa
magunia, wengine walivalia nguo kama askari mgambo, mavuvuzela , filimbi na vifijo vikitawala
nyuso zao zikiwa na michoro kama vikaragosi.
Timu ya Stashahada ya Chuo cha Malya kwanza ilikaguliwa huku timu wenyeji wa Malya Queens
wakigoma kukaguliwana na ikionekana kuwa fainali hiyo sasa inaamuliwa kwa ushindi wa
mezani.

Walipouliza Malya Queens wanalalamikia nini?

“Tuna mashaka na refarii mmoja, kama wanataka tuingia uwanjani
basi atafutwe refa mwingine achezeshe.”

Jambo hilo lilijadiliwa na ikaamuliwa refalii Madawa Lauzi na Lucy Malisa wauchezeshe mchezo
huo. Malya Queens waliingia uwanjani na mchezo ukaanza kwa robo ya kwanza iliyokuwa na
ukame wa magoli ambapo si kawaida ya mchezo wa Netiboli, mchezo huu uliendelea nazo
tambo za pande zote mbili zikiendelea.
Refalii wa ndani ya uwanja Madawa Lauzi aliagiza mashabiki kupunguza kelele kusaidia
wachezaji kusikia vipenga vyake alivyokuwa akivipiga uwanjani hapo kwa umahiri mkubwa, hilo
lilitekelezwa na mashabiki pande zote mbili.
Magoli yalianza kungia pande zote mbili mwishoni mwa robo ya kwanza ambapo hadi robo ya
nne inakamilika Malya Queens walishalala kwa magoli 33 kwa 14 tu kwa hiyo Wanachuo wa
Stashahada wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya wakawa mabingwa.
Ukafika wakati wa kupokea zawadi zikiwamo fedha taslimu kwa mfungaji bora, mshindi wa tatu
kutoka wanachuo wa Astashahada wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya waliopata
sanduku moja la soda, Malya Queens wakiwa washindi wa pili wakipewa mpira wa Netiboli na
wanachuo wa Stashahada ya Michezo Malya wakawa mabingwa wa ligi hiyo ya Netiboli
wakipokea Mbuzi ambapo zawadi zote zimetolewa na mfadhili wa mashindano hayo mkufunzi
Iddi Luswaga.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *